Huku mmiliki wa Klabu ya TP Mazembe, Moise Katumbi, akiendelea kumbania mshambuliaji wa Tanzania, Mbwana Samatta kujiunga na Genk ya Ubelgiji, straika huyo amepanga kuununua mkataba wake uliobakia katika timu hiyo.
Taarifa hizo zimekuja huku kukiwa na madai kuwa Genk iliamua kwenda kushtaki kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kuhusu thamani ya muda wa mkataba wake uliobaki ambapo unatarajiwa kumalizika Aprili, mwaka huu.
Samatta ameshasaini mkataba wa awali na timu hiyo ya Ubelgiji na mpango wake kwa sasa ni kuona anaondoka katika timu hiyo yenye makazi yake katika Jiji la Lubumbashi, DR Congo.
Chanzo cha uhakika kutoka kwa mtu wa karibu na Samatta, kilisema kuwa mpango wa straika huyo kwa sasa ni kununua mkataba wake uliobaki ndani ya timu hiyo ambapo suala hilo tayari ameshamfikishia wakala wake ambaye yupo na mwanasheria kwa ajili ya kulifanyia mchakato jambo hilo.
“Genk wamekwenda Fifa kushtaki lakini kwa upande wa Samatta, amemuagiza wakala wake akae na mwanasheria kwa lengo la kujadili jinsi ya kununua mkataba wake uliobaki ili aweze kuondoka,” kilisema chanzo hicho.
Kwa upande wa meneja wa mchezaji huyo, Jamali Kisongo alipoulizwa kwanza alikiri kuwepo kwa mpango huo wa kununua mkataba uliobaki kwa kuwa hawafikirii kukubali mchezaji kurejea Mazembe.
“Ni kweli huo mpango wa kununua sehemu ya mkataba wake upo, umeshaanza kufanyiwa kazi kupitia wakala na mwanasheria wake licha ya Genk kwenda Fifa, lakini sisi tunaangalia namna ya kuweza kulishughulikia kwa sababu hata atakaporejea kutoka kwenye tuzo huko Nigeria, tutasafiri kwenda Ubelgiji kukamilisha mambo yaliyobakia likiwemo suala hilo la mkataba,” alisema Kisongo.
0 COMMENTS:
Post a Comment