Mshambuliaji wa Simba, Mkenya, Paul Kiongera, ametamka kuwa, hata yeye binafsi anashangazwa na kiwango kibovu alichonacho sasa cha kushindwa kufunga bao lolote akiwa na kikosi hicho, licha ya kutoka kufanya vyema alipokuwa na KCB ya Kenya.
Kiongera alirejeshwa Simba kuja kusaidiana na mastraika wengine waliopo ndani ya kikosi hicho akiwemo, Hamis Kiiza ambapo licha ya kucheza katika michezo kadhaa mpaka sasa, hajafanikiwa kufunga bao lolote lile.
Kiongera ambaye alipata majeraha ya msuli kwenye mchezo dhidi ya JKT Ruvu, amesema kuwa licha ya kucheza kwa kiwango cha juu lakini anashangazwa na ubutu alionao wa kushindwa kupachika mabao licha ya kupata nafasi nyingi za kufunga.
“Unajua hata mimi mwenyewe najishangaa kabisa juu ya hili tatizo la kufunga ambalo limenipata ghafla tangu nitue Simba tofauti na ilivyokuwa KCB ambapo nilikuwa nikifunga mabao mengi sana.
“Lakini sitaki kusema kuwa hali hii imechangiwa na ushirikina (misumali) kwani huwa napata nafasi nyingi za kufunga ila nashindwa kumalizia tu, ila najipanga zaidi kuhakikisha nalitatua tatizo hili haraka sana kabla ya raundi ya pili ya ligi ambapo nimepanga kuwa moto katika ufungaji,” alisema Kiongera.
Kwa upande mwingine, Kocha wa Simba, Jackson Mayanja, amesema Kiongera anahitaji msaada ili arejee kwenye kiwango chake.
“Mimi sijakaa naye kwa muda mrefu Kiongera tangu nifike, lakini ni mmoja kati ya wachezaji wazuri ndani ya Simba na ana umbo kubwa ambalo akilifanyia kazi atakuwa bora zaidi.
“Siwezi kumuacha hivihivi apotee ni lazima nitumie jitihada zangu kuweza kumuandaa kikamilifu ili aweze kurejea katika kiwango chake kwani ni mchezaji mwenye umbo zuri na ni mkubwa, hivyo iwapo atasaidiwa basi ni wazi atakuwa mchezaji mzuri,” alisema Mayanja.
0 COMMENTS:
Post a Comment