KAKA WA MBWANA SAMATTA, MOHAMMED SAMATA |
HAKUNA asiyefahamu kama Mtanzania, Mbwana Samatta ndiye Mchezaji Bora wa Afrika kwa wanaocheza ndani kwa mwaka 2015. Hiyo ilithibitika usiku wa kuamkia Ijumaa iliyopita katika Jiji la Abuja, Nigeria.
Katika sherehe hizo za utoaji tuzo mbalimbali zilizoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Samatta alikuwa kwenye kipengele hicho kimoja akiwania tuzo binafsi, lakini mbali na kuinyakua tuzo hiyo, alichaguliwa katika kikosi bora cha Afrika akiwa na nyota kama Yaya Toure na Pierre-Emerick Aubameyang.
Samatta pia akachukua tuzo ya jumla kutokana na klabu yake ya TP Mazembe kutoka DR Congo kuchaguliwa kuwa timu bora kwa mwaka huo.
Tuzo binafsi ya Samatta, alikuwa akishindana na Mcongo, Robert Kidiaba anayeichezea TP Mazembe na Mualgeria, Baghdad Bounedjah wa Etoile du Sahel.
Mohammed Samata ni kaka wa Mbwana ambaye anakipiga katika timu ya Mgambo JKT ya Tanga.
Kuhusiana na kile kilichotokea mpaka mdogo wake huyo kuitwaa tuzo hiyo, Samata anasema.
“Awali ya yote kwanza tuzo hiyo ni kitu ambacho hakijawahi kutokea kwa mchezaji yoyote kutoka Tanzania kuwahi kufanya hivyo, kutokana na hilo ni wazi ameipa nchi heshima lakini pia yeye mwenyewe imemjengea sifa na jina.
“Kujitambua kwake na kujituma ndiyo silaha iliyofanikisha haya yoye na matunda yake yameonekana, amethubutu na ameweza, siku zote kuthubutu ndiyo njia sahihi ya kufanikiwa.
SAMATA (KULIA) AKIITUMIKIA MGAMBO DHIDI YA YANGA KATIKA LIGI KUU BARA. |
“Nakumbuka wakati anajiandaa na safari ya kwenda Nigeria kwenye tuzo hizo, nilikaa naye na kuzungumza mambo mengi sana, kati ya hayo nilimwambia nenda Nigeria ukachukue tuzo yako usiwe na wasiwasi kwani nilikuwa nikiamini kwamba uwezo wa kufanya hivyo anao kutokana na wale aliokuwa akishindana nao kuonekana hawana uwezo wa kumshinda.
“Nilimwambia kama kungekuwa na uwezekano, ile tuzo ingepandishwa ndege tu ije Bongo bila hata ya kufanyika kwa sherehe, lakini kutokana na utaratibu ulivyopanga, haikuwa na jinsi mpaka akaenda kule na kurudi nayo.
“Wakati anarejea nilitamani niwepo katika eneo la tukio ili nimpokee, lakini kutokana na kubanwa na majukumu ya timu yangu nilishindwa kuwepo.
“Nilijisikia vibaya kukosa kumpokea, lakini kwa kuwa nilijua mapema atarudi na tuzo hiyo basi nilijiandaa kwa hilo, lakini mara ya kwanza wakati anarudi Tanzania baada ya kuiwezesha klabu yake ya TP Mazembe kuchukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, nilienda kumpokea, kwa kweli nilifarijika sana, hivyo safari hii kukosa kumpokea nikaona kawaida japo nilitamani.
“Safari yetu ya soka tulianza wote tangu tukiwa wadogo, siku zote mkubwa ni mkubwa tu, hivyo kutokana na mimi kuwa mkubwa kwake kila sehemu tuliyokuwa tukienda kucheza nilikuwa nikipata nafasi na yeye anasubiri, lakini kiukweli tangu utotoni kwetu yeye alikuwa na kipaji kuliko mimi.
“Katika kusaka mafanikio hakuna kulazimisha jambo na vitu vingine huwezi kuvizuia kutokea kutokana na kila siku unaona jinsi mambo yanavyokwenda na katika kundi la watu wengi basi mmoja anaonekana kuwa juu zaidi ya wengine. Hali hiyo ndiyo ilikuwa kwa Mbwana, yeye alionyesha dalili mapema ya kufika mbali, na leo ndiyo huyu tunamzungumzia hapa.
“Mdogo wangu amepiga hatua kubwa kisoka kuliko mimi lakini kwa upande wangu siwezi kuyazungumzia matarajio yangu ya hapo baadaye, nimeamua kuuachia muda wenyewe ndiyo uzungumze kwani naweza kusema hivi kumbe muda bado haujafika, lakini muda ukifika kitaeleweka tu, kwa sasa naendelea kupambana mwenyewe tu hadi nione mwisho wake.
Familia yao
“Katika familia yetu tumezaliwa watoto sita wa baba mmoja, mama mmoja, wa kwanza anaitwa Rajabu ambaye kwa sasa ni mwalimu na anafundisha shule moja ya msingi huko Mbeya, wa pili ni Mukhsin (mwanajeshi na anaishi Dar), watatu anaitwa Saad (Ofisa Polisi anaishi Dodoma, wanne Saidi (mfanyabiashara, anaishi Dar), wa tano mimi na wa sita Mbwana. Lakini kwa upande wa mama mwingine yupo dada yetu anaitwa Sophia, anaishi Dar.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment