January 2, 2016


Na Saleh Ally
KOCHA Jose Mourinho ameondoka Chelsea huku akiacha gumzo kubwa na sasa kikubwa kinachojadiliwa ni namna ambavyo wachezaji walilenga kumsaliti, mwisho wakaonekana kufanikiwa.

Suala la usajili, linaweza kulingana na dhambi ya uzinzi kwani mambo yake hufanyika kwa siri kubwa na mara nyingi watendaji huwa na visingizio vingi, halafu pia ushahidi wake huwa ni mgumu pia.

Mashabiki wa Chelsea waliingia uwanjani na mabango wakiwazodoa wachezaji ambao wanaamini walikuwa ni wasaliti licha ya Mourinho raia wa Ureno kuwanunua kwa fedha nyingi ili waisaidie Chelsea.
Kuondoka huku wengi wakiamini Mourinho alisalitiwa, kusalisababisha wengi wasahau kujadili mafanikio na kufeli kwake kwa hali halisi.

Hii ni mara ya pili Mourinho anaondolewa Chelsea baada ya ile mwaka 2004 akitokea FC Porto, halafu mwaka 2007 mambo yakawa magumu akaachishwa kazi ingawa mpango ulikwenda kishikaji kati yake na mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich.

Safari hii, Mourinho alirejea Chelsea akitokea Real Madrid, ilikuwa ni mwaka 2013, msimu wa kwanza mambo hayakuwa mazuri, msimu uliofuata akabeba ubingwa lakini msimu wa tatu amefungashiwa virago hata kabla ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu England!
Kweli Mourinho ni kocha mkubwa, ukiachana na suala la kuhujumiwa na kumhukumu au kumjadili kwa maana ya fedha alizotumia kwa usajili pamoja na matokeo uwanjani, utaona kikosi chake hakikuwa na mambo mazuri safari hii ukilinganisha na kile kipindi cha 2004-2007.


Usajili:
Rekodi ya matumizi ya fedha zinaonyesha kwa vipindi vyote viwili alivyokuwa Chelsea, Mourinho alitumia jumla ya pauni milioni 515.4 kwa ajili ya usajili.
Fedha hizo ni zaidi ya zile alizotumia Arsene Wenger wa Arsenal kwa kipindi cha miaka 19 na nusu msimu akiwa na timu hiyo. Akiwa na Arsenal kwa kipindi hicho, Wenger ametumia pauni milioni 515.2.
Kwa maana ya mafanikio, utaona kweli Mourinho amepeleka heshima kubwa Chelsea kwa kubeba makombe mfululizo kwa vipindi vyake na hauwezi kumhukumu.

Ingawa usajili wa fedha nyingi wa kipindi hiki alichotimuliwa akiiacha timu katika nafasi ya 15 katika msimu wa ligi, zinaonekana hazikumsaidia.
Kipindi cha 2004-2007, Mourinho alisajili wachezaji kwa bei ya juu pia, lakini kwa kiasi kikubwa walifanya vema na kuwa msaada mkubwa kwake. Mchezaji pekee aliyemsajili kwa fedha nyingi sana ni Andrey Shevchenko ambaye hata hivyo inaonekana hakumfurahia sana, lakini Abramovich alitaka iwe hivyo, wakatoa pauni milioni 30 kwa AC Milan ili kumnasa nyota huyo, lakini hakutamba sana.

Mchezaji wa pili kuwa ghali kipindi hicho alikuwa ni Michael Essien aliyenunuliwa kwa pauni milioni 24.4, akafuatiwa na Didier Drogba ambaye walimtoa Marseille kwa pauni milioni 24. Pia Chelsea ikatoa pauni milioni 21 kumnasa kiungo Shaun Wright-Phillips, Ricardo Carvalho naye akanunuliwa kwa pauni milioni 19.5 naye akawa msaada mkubwa.

Katika kipindi cha pili ambacho kinaanzia mwaka 2013-15, Mourinho alisainisha wachezaji wengi lakini hawa watano ndiyo walikuwa ghali zaidi.

Diego Costa aliyenunuliwa kwa pauni milioni 32, Willian (pauni milioni 30), Cesc Fabregas (pauni milioni 27), Jose Cuardrado (pauni milioni 23.3) na Pedro Rodriguez kutoka Barcelona waliyempata kwa kitita cha pauni milioni 21.4.
Usajili ghali zaidi wa kipindi hiki, unaonyesha kutomsaidia zaidi Mourinho kama ule wa nafuu wa kipindi cha kwanza.


Takwimu:
Mourinho kaondoka Chelsea takwimu zikiwa zinambana sana hasa kama utalinganisha kwa vipindi vyake viwili akiwa na Chelsea.

Kipindi 2004-2007:
Katika kipindi hicho, Mourinho aliingoza Chelsea kucheza mechi 185. Akashinda 124, akapata sare 40 na kupoteza 21 tu.

Katika kipindi hicho alipata wastani wa kushinda wa asilimia 67.03 kwa maana ya ubora.
Wakati anaondoka alikuwa amechukua ubingwa wa Ligi Kuu England mara mbili, Kombe la FA, mara moja, Kombe la Ligi akabeba mara mbili pia Ngao ya Jamii.

Kipindi 2013-2015:
Katika kipindi hiki, Mourinho alirejea na kuikuta Chelsea ikiwa haipo katika kiwango kibaya sana, msimu mzima wa kwanza akaambulia ziro.
Hadi anaondoka, ameiongoza Chelsea katika mechi 161 ikiwa ni tofauti ya uchache wa mechi 24 tu ukilinganisha na kipindi cha kwanza cha kati ya mwaka 2004-2007.

Katika kipindi cha pili, Mourinho alishinda mechi 89, sare 33 na akapoteza 39.
Ukiangalia kipindi cha kwanza, utagundua cha pili alifeli zaidi, huenda watu wamejua mbinu zake au hujuma zilimzidi nguvu.

Wingi wa mechi za kupoteza umekuwa juu, sare zimeongezeka na ushindi umepungua ndiyo maana wastani wa kushinda ulikuwa ni asilimia 55.28 ukilinganisha ya 67.03 ya kile kipindi cha kwanza.

Kama hutajali na kuangalia sana fedha alizotumia na kumzidi hata Wenger ambaye amekuwa Arsenal tangu mwaka 1998 alipotokea Grumpus Eight ya Japan, utagundua kuna mambo mawili makubwa.


Kwamba fedha inaweza kusaidia mambo yakabadilika na kuleta mafanikio. Kwa kuwa kwa vipindi vyote viwili, Mourinho alibeba makombe saba ya Ligi Kuu England, FA na Ligi, pia akabeba ngao moja.


Kama utalinganisha na kipindi cha Wenger, utaona yeye Mourinho ni mwenye mafanikio. Lakini cha pili cha kujifunza, fedha si kila kitu, kuna wakati unafeli hata zikiwa nyingi na kama kutakuwa hakuna moja. Hilo ndilo lililomkuta Mourinho na linaweza kuwa funzo Ulaya au hata hapa nyumbani Tanzania.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic