Na Saleh Ally
TUMEELENDELEA na mahojiano na mshambuliaji wa TP Mazembe, Mbwana Ally Samatta kwa wiki moja sasa na hii ni sehemu ya mwisho ya mahojiano hayo.
Samatta amekuwa na mafanikio makubwa ukilinganisha na vijana wanamichezo wengine wa Kitanzania. Ameiongoza TP Mazembe ya DR Congo kubeba ubingwa wa Afrika, kucheza Kombe la Dunia la Klabu.
Sasa ameingia tatu bora ya wachezaji wanaowania tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika kwa wale wanaocheza barani Afrika.
Amekuwa ni mfano wa kuigwa, mpambanaji ambaye wengi wangependa kusikia njia aliyopita kufikia hapo na malengo yake.
Mwisho ilikuwa Jumamosi ambapo alikuwa ameulizwa swali kuhusiana na uamuzi wake wa kwenda Ulaya ambako ataanza moja. Amejipangaje? Endelea.
SALEHJEMBE: Sasa umeamua kwenda Ulaya, umeshaonana na uongozi wa Genk, mshahara wako au maslahi yako yatazidi kwa kiasi gani yale ya TP Mazembe?
Samatta: Hatua maana yake ni kuongezeka kwa maslahi, au malengo ya unachotaka kufanya, lakini sitasema kuhusu mshahara.
SALEHJEMBE: Unakwenda kuanza upya wakati tayari Mazembe ulikuwa staa, kumbuka uliishi maisha ya hofu baada ya kufika Lubumbashi. Umejiandaaje?
Samatta: Nina uzoefu na mambo yalivyokuwa Mazembe, ugumu wa kule nitaurudisha uzoefu wa changamoto nilizozipata Congo na kuanza nazo Ubelgiji, ninaamini nitafanikiwa.
SALEHJEMBE:Tayari wewe ni staa, Ubelgiji utakuwa ni mtu usiyejuana na yeyote, usiyejulikana na watu hawatakujali kabisa?
Samatta: Kweli, nalitegemea hilo lakini sitakwenda kule kama staa, nakwenda kuanza upya, nalitambua hilo. Nitapambana ili nidhaminike kwa ubora wa kazi yangu kama ilivyokuwa Mazembe. Najua hakuna atakayenijali, hata kama nilisikika Afirka lakini najua Ulaya wengi hawajui kuhusu Afrika.
SALEHJEMBE: Kwa kuwa umezungumza na Genk utakuwa unajua utalipa mshahara kiasi gani. Lakini kodi kubwa za Ulaya zinaweza kukufanya usiwe na tofauti yoyote na Mazembe ulipokuwa ukilipwa dola 15,000?
Samatta: Kweli, lakini huu si wakati wa kujali kila kitu kuhusu mshahara na maslahi kwa jumla, niliangalia suala hilo. Najua kabisa kabla ya kodi ni kiasi gani na baada ya kodi ni kiasi kipi na tofauti yake na Mazembe ni ipi. Mikataba ya Wazungu iko wazi kwa kila kitu.
SALEHJEMBE: Labda inaweza ikawa inazidi kiasi gani mshahara unaopata Mazembe kipindi hiki?
Samatta: Ni siri.
SALEHJEMBE: Umefikia hapo ulipo, lakini inaonekana asilimia 90 ya vijana wa Kitanzania wamekwama kabisa, unafikiri tatizo ni nini au unawazidi kwa kiasi gani?
Samatta: Kwa mimi ninavyowaona wachezaji wengi, hakika wanaweza kwa asilimia 90 kucheza Congo, Afrika Kusini na kwingineko.
SALEHJEMBE:Kama ni hivyo, tatizo ni nini, nirudie unafikiri unawazidi nini?
Samatta: Sidhani kuna tofauti kubwa kati yangu na wao, hakuna kikubwa ninachowazidi. Inawezekana ni suala la kujituma tu na kuamini utaweza jambo fulani. Hautaweza kitu hadi uamini utaweza na ufanye kwa vitendo tena kwa kujituma.
Wakati mwingine nasema huenda wako wana nia ya kufanya vizuri, lakini tatizo kubwa kwao inakuwa ni kupata nafasi. Bado juhudi zinaweza kumpa mtu njia na mwisho akapata nafasi.
SALEHJEMBE: Miaka 23, sasa unakwenda 24, tena ni mwanamichezo staa, vipi kuhusiana na kutengeneza familia?
Samatta: Familia ipo, kama unavyoona wazazi na ndugu zangu pia.
SALEHJEMBE: Nina maanisha kufunga ndoa?
Samatta: Aaah, kwa sasa hilo bado kabisa. Nafikiri nitafanya hivyo pale nitakapokuwa nimetulia kidogo. Kama nitakuwa ninacheza soka halitakuwa la ushindani sana wakati huo. Unajua maisha ya wanasoka ni kutangatanga hautulii kabisa. Ningependa kufunga ndoa katika kipindi ambacho nimetulia.
SALEHJEMBE: Unafikiria kufanya hivyo baada ya miaka mingapi?
Samatta: Nafikiri mitano hadi saba Mwenyezi Mungu akijaalia. Angalau nikiwa nimefikisha miaka 30, nafikiri utakuwa ni wakati mzuri wa kuliangalia hilo ili nilitendee haki kwa asilimia kubwa.
SALEHJEMBE:Wewe ni shabiki wa timu gani katika soka la ushindani la Ulaya?
Samatta: Mimi ni shabiki mkubwa wa Manchester United, ingawa kwa kipindi hiki mambo hayaendi vizuri, lakini ndiyo mambo ya soka.
SALEHJEMBE: Ukijaaliwa kuendelea kwa kiwango cha juu kabisa, ungependa kuichezea timu gani ambayo ndiyo ndoto yako kama timu kubwa zaidi?
Samatta: Awali nilipenda sana iwe Manchester United, lakini baadaye mambo yalibadilika. Kwa sasa ningetamani sana siku moja kuvaa jezi ya Barcelona.
SALEHJEMBE: Kwa nini Barcelona na si Manchester United kama ulivyokuwa ukitamani hapo awali?
Samatta: Kila binadamu anapenda mafanikio, hata kama utayakuta sehemu basi uyaendeleze. Nafurahishwa na mwenendo wa Barcelona, naona ni watu makini, wanaojituma, wasiochoka ndiyo maana wanafikia hapo walipo.
SALEHJEMBE: Kwa kipindi hiki cha mapumziko, umepanga kufanya lolote nje ya soka?
Samatta: Hapana itakuwa ni mapumziko hapa nyumbani, pia nitaendelea na mjadala kuhusiana na suala la kuhamia Ulaya, bado TP Mazembe hawajamalizana na Genk. Hivyo ni suala la kuvuta subira hadi siku nitakapopata uhakika.
MWISHO
0 COMMENTS:
Post a Comment