LYANGA |
Na Saleh Ally
KAMA ni rekodi zinaonyesha Alex Ferguson ndiye kocha mkubwa na bora zaidi kuwahi kutokea katika historia ya soka la England.
Rekodi ndizo zinazombeba, kwani kabla ya kustaafu rasmi ukocha Mei 2013, Alex Ferguson aliifundisha Manchester United na kuibadilisha iwe klabu maarufu, tajiri na tishio uwanjani kuliko nyingine zote za England.
Alishinda mataji 13 ya Ligi Kuu England ikiwa ni zaidi ya nusu ya utajiri wa makombe hayo kwa klabu hiyo lakini akashinda mengine mbalimbali 25.
Ukirejea katika biashara, Ferguson alikuwa ni zaidi ya kocha, alicheza kama kiungo mchezeshaji wa gurudumu la maendeleo ya Manchester United. Kwani kuna ule msemo usemao hivi: “Apple ni Steve Jobs” na “Manchester United ni Sir Alex Ferguson.”
Mwaka 2012, Chuo Kikuu cha Harvard ambacho ni kikubwa na maarufu kiliamua kufanya uchunguzi wa ung’amuzi wa masuala ya kibiashara kupitia utendaji kazi wa Ferguson kuona aliweza vipi kufanya aliyoyafikia pamoja na presha kubwa ndani ya mchezo wa soka, kutoka kwa viongozi, wachezaji na mashabiki, jambo ambalo limewashinda watu wengi sana.
STEVE JOBS |
Profesa Anita Elberse anayetokea katika kitengo cha biashara cha Havard ndiye ameamua kujifunza na kuandika kazi ya Ferguson. Tayari wawili hao wamekutana na kazi imeanza ikiwa ni pamoja na kuwahoji watu mbalimbali waliofanya kazi na kocha huyo. Watahojiwa wachezaji, mashabiki, viongozi lakini makocha na wengine wengi, huku yeye akieleza matatizo na misimamo aliyoitumia kufikia malengo.
Hii nilikuwa kama ninakumbusha tu namna ambavyo watu waliofanikiwa wanavyoweza kupita katika maeneo magumu yenye ushindani na upinzani mkubwa. Wakiendelea kufanya wanachokiamini, mwisho hufanikiwa na kufanya makubwa ambayo baadaye hugeuka kuwa gumzo au mifano ya baadaye kwa maisha ya wengine.
Nimepanga kumlenga mshambuliaji Danny Lyanga wa Simba, kijana ambaye alianza kwa kasi kubwa Msimbazi lakini katika mechi kadhaa akaonekana kupoteza mwendo “balansi” hali ambayo iliwashtua wafuatiliaji wengi wa mambo na kuanza kusema, alianza kwa kasi, mwisho anapotea.
Wako walioanza kumtolea mfano na yule Mliberia wa zamani wa Yanga, Kpah Sherman, kwamba baada ya mechi moja dhidi ya Simba, hakuwahi tena kurudi!
Juzi, Lyanga amefunga bao lake la pili ndani ya mechi sita za Ligi Kuu Bara akiichezea Simba. Alifunga mara ya kwanza dhidi ya Toto Africans, bao safi kabisa lakini Simba ikamaliza na sare ya 1-1.
Bao la pili hiyo juzi dhidi ya JKT Ruvu, safari hii alifunga bao jingine safi akimpangua kipa na kuacha mpira uende taratibu kugusa nyavu.
Kwangu Lyanga ni mchezaji mwenye kipaji cha juu kabisa ambacho kikishikiliwa na yeye na walio karibu yake, basi ni lulu ambayo itakuwa faida si kwa Simba tu, badala yake taifa zima.
ALEX FERGUSON |
Kikubwa ni lazima Lyanga ndiye awe mlezi wa kwanza wa kipaji chake, pia mshika tochi ya dira kwamba anaelekea wapi bila ya kujali nani anasema nini kama ambavyo Ferguson aliamua kufanya.
Lyanga alipoteza nafasi nyingi katika mechi dhidi ya Mwadui, halafu Mtibwa, akafanya hivyo katika mechi dhidi JKT kabla ya mwisho kufanikiwa kufunga. Ukimuangalia utajua ni mtu aliyepania, au hayuko vizuri kisaikolojia au ana presha inayomkoroga kutaka kuonyesha makali.
Vizuri akawa aliye na malengo, ambaye anataka kufanya kitu kwa malengo sahihi, kutaka kufikia anachokiamini. Hii haikatazi kuchukua ushauri, lakini kuuchuja na kuangalia sahihi ni upi ni jambo sahihi.
Lyanga bado ana nafasi ya kubadili uchezaji wake kwenda kwenye ubora kwa kufanya mazoezi zaidi, awe na pumzi na imara zaidi. Anahitaji kujifunza kwa kuangalia ikiwezekana hata video zaidi za uchezaji wa nyota mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.
Kwa jicho la kwanza, kipaji chake ni zawadi kuu, kimo amepewa, ana kasi na akili ya haraka ya kufanya uamuzi. Vyote vinafunikwa na papara inayojengwa na presha.
Sasa baada ya bao la juzi, vizuri akaviua vyote vinavyofunika alivyonavyo na kutengeneza njia sahihi kama aliyojiwekea Ferguson ambaye hadi anastaafu, anaonekana ni bora zaidi kuliko mwingine yeyote. Mimi ninaamini Lyanga akitulia, asivimbe kichwa, akafuata anachoamini ni sahihi, akaweka jitihada na kuamua kusonga, atakuwa hakamatiki na muda wa kubaki Tanzania utakuwa mchache huku akiacha gumzo hapa nyumbani.
0 COMMENTS:
Post a Comment