January 25, 2016



Aliyekuwa kocha wa Simba, Dylan Kerr ameandika waraka kwa vyombo vya habari na na mashabiki wa Simba kuelezea mambo mbalimbali yaliyotokea katika klabu hio ndani ya muda wa miezi sita aliyokaa.


” Wapenzi na Mashabiki wa Simba Sports Club,

Huu ni waraka wangu rasmi na tamko langu la mwisho kwa vyombo vya habari na mashabiki wa Simba Sports Club.

Uongo mwingi umezungumzwa, na kuna wakati zimetolewa kauli za kuumiza kwenye vyombo vya habari kunihusu mimi na kazi yangu katika timu ya Simba, hivyo basi waraka huu utakuwa ni wakujitosheleza juu ya hoja zilizotolewa.

Ninajisikia vibaya sana kuona nimekuwa na mwisho wa ghafla kiasi katika Klabu hii.

Miezi sita niliyokuwepo Simba SC iligubikwa na changamoto nyingi za kimwili na kiakili, lakini pamoja na hayo niliweza kufurahia maisha.

Mashabiki wa Simba SC na Watanzania wote kiujumla nimeishi nao vizuri, wamenikarimu na kunifanya nifurahie maisha na kuifurahia nchi nzuri ya Tanzania.

Nilikuwa nina mkataba wa miaka miwili na timu ya Simba SC, mkataba ulio bayana na wa kisheria, “ningehukumiwa kwa nafasi yangu katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom mwishoni mwa msimu 2015-2016 (kushinda lilikuwa jukumu langu) na utendaji kazi wangu katika ligi ya mabingwa barani Afrika 2016-2017 ambayo tulikuwa na uwezekano mkubwa wa kushiriki”.

Katika mkataba wangu, hakuna mahala palipoainishwa utendaji kazi wangu kwenye mashindano ya kombe lolote, hata mashindano ya hivi karibuni huko Zanzibar hayakuelezwa kama moja ya mashindano yatakayopima kazi yangu.

Ninaamini pasipo na shaka, kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, huku tukiwa na uwezekano mkubwa wa  kupanda nafasi ya pili au ya kwanza, nilikuwa mbioni kufikia malengo yaliyowekwa na uongozi wa timu.

Nimekuwa kwenye fani hii kwa miaka 32, nimecheza ligi kubwa Uingereza na kupata mafanikio kama mchezaji, lakini kadhalika nimepata mafanikio katika nyanja ya ualimu wa mpira.

Nina sifa za kutosha na weledi wa hali ya juu, nina beji za shirikisho la soka barani Ulaya (UEFA), pamoja na uzoefu mkubwa katika nyanja ya mpira wa miguu bila kusahau ngazi ya timu ya Taifa.

Mimi sio aina ya mwalimu anayeweza  kufanya kazi huku akiingiliwa na watu wasioujua mpira, wasio na vyeti, wasio na uzoefu, wasiokuwepo katika bodi ya mpira wa miguu, ambao sio tu kwamba wanataka kuwa juu ya timu, bali pia wahusike na majukumu ya kusajili na kufukuza wachezaji na kimsingi hili haliwezi kuiendeleza timu.

Vilevile, wimbi kubwa la waalimu walioajiriwa na Klabu ya Simba kwa miaka ya hivi karibuni inaonesha dhahiri kuonesha mahala tatizo lilipo, Klabu inatakiwa kufanya maamuzi magumu, pia kubadili utamaduni huu haraka iwezekanavyo vinginevyo timu hii haitaendelea na badala yake watazidi kurudi nyuma.

Klabu nzima ya Simba imekuwa haina kiongozi hata mmoja mwenye cheti cha Mpira kinachotambuliwa na vyama kama UEFA au CAF, ni kwa mara ya kwanza kiongozi mmoja tu hivi karibuni amehitimu mafunzo ya awali ya ualimu wa mpira.

Klabu hii itazidi kuporomoka kama haitampata na kumteua kiongozi mmoja aliye na cheti kinachotambuliwa na CAF au UEFA na mwenye uzoefu wa kutosha katika fani ya mpira ili afanye kazi karibu na mwalimu katika masuala ya usajili, mipango ya mchezo, maandalizi ya ligi, vifaa vya mazoezi, mkakati wa kuendeleza soka la vijana na mambo yote yahusuyo ufundi.

Wadhifa wa “mkurugenzi  wa ufundi” ni muhimu sana, wakati CAF ikiendelea kushughulikia leseni mpya za uendeshaji wa klabu barani Afrika, Klabu ya Simba inatakiwa kuhakikisha inakuwa na mfumo sahihi wa kiutawala ili kuweza kufuzu kuipata leseni hii.

Ingawa  nimekutana na matatizo ya kutolipwa mishahara, kwangu mimi na kwa wachezaji wangu hasa mwezi Novemba na Desemba, niliendelea kufanya kazi yangu na nilijitoa kwa moyo mmoja.

Nimefanya kazi katika medani ya mpira wa miguu kwa maisha yangu yote, naelewa mambo kama haya hutokea, lakini  mimi na wachezaji  tulijikuta tunalazimika kuvumilia manyanyaso kutoka kwa baadhi ya viongozi, siamini kama ilikuwa ni sahihi na sio  weledi wa kazi.

Ni kweli, sote hatukupendezwa na mashindano ya hivi karibuni mjini Zanzibar, kupoteza mchezo katika hatua ya nusu fainali, lakini ikumbukwe kwamba lengo langu lilikuwa wazi na mamlaka yangu yanajulikana, Ligi kuu ilikuwa muhimu zaidi na tulitumia mashindano ya Zanzibar kukitazamia kikosi kizima na kuwapa nguvu mpya wachezaji ili tuweze kukabiliana na ligi na hatimae kufikia mafanikio.

Kusikia kwamba “timu haikuwa fit” hiki ni kichekesho, kucheza mechi mfululizo, kusafiri kwa basi zaidi ya saa 25, ni kweli wote tulikuwa tumechoka lakini “kutokuwa fit” ni hoja ya mzaha kabisa.

Mwalimu wa viungo hakufukuzwa, isipokuwa mkataba wake wa miezi mitatu ulipokwisha hakuongezewa, na kutokana na tabia zake katika masuala kadha wa kadha  haikushangaza kutokuwa nae.

Klabu ya Simba haitakiwi kufumbia macho baadhi ya viongozi wanaoichafua heshima ya Klabu, ambao kwa makusudi wanamuua kuitia aibu timu hii kwa kutofuata taratibu zinazotakiwa hasa wanapoiwakilisha timu.

Jambo la msingi zaidi ambalo nataka kuliweka sawa ni kuhusu mwalimu wa viungo mbalo limekuwa likizungumzwa mara kwa mara, wapenzi na mashabiki wa Klabu Simba ni lazima wafahamu ukweli kuhusu mwalimu huyu.

Nilipendekeza kwa uongozi waalimu wengi wa viungo wenye utalaamu na sifa za kutosha, walio na beji za UEFA na CAF katika Nyanja ya viungo (lakini hakupatikana), ingawa hata mimi nimefuzu katika eneo hili kwa maana ya vyeti vyangu vya UEFA, na ningeweza kufundisha bila mwalimu wa viungo na hili lingesaidia sana kuokoa fedha za Klabu zisiende bure.

Niwe mkweli tu, baada ya mazoezi yote ya msingi tuliyofanya wakati tunajiandaa kuanza Ligi kuu, hatukuhitaji kuwa na mwalimu wa viungo kama sehemu ya waalimu wa timu hasa ukizingatia ratiba ilivyokuwa, ni michezo miwili tu kwa juma.

Nimekuwa nikiusumbua uongozi kuhakikisha nyasi za uwanja wa Taifa zinakatwa ili kuhakikisha mtindo wetu wa upigaji pasi unaendana na hali ya uwanja, mtindo ambao mimi na jopo langu tulikuwa tunajaribu kunamaliza maneno juu ya wachezaji.

Urefu wa nyasi kwa mara nyingine ulikuwa hatari sana kwa wachezaji , ambao wamekuwa wakipata majeraha makubwa,  ni jukumu la Klabu yeyote ya mpira inayoendeshwa kiuweledi kuhakikisha inatilia maanani masuala muhimu hasa linapokuja la ustawi wa timu kwa maana ya wachezaji.

Kuwa na msaada kwa mwalimu wa timu na kwa wachezaji, ni pamoja na kuhakikisha masuala madogo madogo yanayoombwa yanatekelezwa.

Lakini pia nimekuwa nikiomba katika michezo yetu tutumie mipira bora na halisi ya Adidas badala ya mipira isiyo na kiwango bora, lakini baadhi ya viongozi walitulilazimisha kutumia mipira isiyo na ubora ambayo hata wachezaji waliichukia na hawakutaka kuitumia, lakini ilitulazimu kwani viongozi wale walifanya ili kutimiza matakwa ya mtu mmoja.

Inashangaza sana kuona baada ya mimi kuondoka tu, nyasi za uwanja wa Taifa zimekatwa na mipira halisi ya Addidas imeanza kutumika.

Nasema Bravo Simba!!!!

Kama ambavyo Ce Ce Peniston aliimba “finally”

Lakini najiuliza kwanini iwe sasa hivi?? Baada ya michezo 14 ya msimu huu.

Tuachane na hayo, binafsi napenda kusema haya yafuatayo;-

Niwashukuru mashabiki wote na wanachama wa Simba Sports Club ambao mliniunga mkono na kunijali, nisingeweza kumridhisha kila mmoja wetu, lakini huo ndio mchezo wa mpira ulivyo.

Wanasimba ni watu wenye mapenzi na timu yenu na mnajitolea sana.

Pia napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na vituo vya misaada ambavyo wachezaji na wafanyakazi wote wa Klabu ya Simba tulivitembelea sehemu mbalimbali ya nchi nikiwa kama Kocha mkuu wa Klabu, nilifarijika na kufurahi kufika maeneo hayo.

Shukrani kwa Dereva wangu Dula, benchi la ufundi, na kikosi maridadi cha wachezaji wote wa Simba SC ambao walifanya kazi kwa kujituma sana, nitawakumbuka sana.

Kwa Rais wa Klabu ya Simba, namshukuru kwa dhati kwani  mara zote amekuwa akiniunga mkono, nashukuru kwa nafasi uliyonipatia na pia shukrani zangu ziende kwa baadhi ya viongozi ambao walijaribu kuniunga mkono.

Kwa kuongezea tu,  naweza kusema Rais wa Simba SC aliagiza nilipwe mishahara yangu, na ninathibitisha nimelipwa stahiki zangu zote kama tulivyokubaliana katika mkataba.


Nimeiacha timu katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, nautazama muda wangu ndani ya Simba kwa hisia mchanganyiko. Nilikamilisha nusu ya kazi.

Mwisho kabisa, kwa Wanasimba na Watanzania wote, niewatakie maisha mema na kila la kheri.

Ahsanteni Sana.

Dylan Kerr.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic