January 26, 2016


Na Saleh Ally
Unawezaje kuwa mdau wa michezo unayetaka maendeleo ya soka nchini halafu ukaamini kweli Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linaweza kusaidia yapatikane? Utakuwa mpuuzi.

Inawezekana kabisa hata kuamini TFF ni jina zuri au linalovutia, unaweza kuwa ni ujinga mwingine. TFF ni tatizo na mdudu anayechangia soka nchini kuporomoka.

Huenda bila TFF Tanzania ingecheza Kombe la Mataifa Afrika au Kombe la Dunia. Lakini kwa hali ilivyo sasa, acha hadithi ihadithiwe juu ya hadithi.

Umesikia lile sakata la kila timu ya Ligi Kuu Bara kuamua kuachana na ligi hiyo kwa muda, ili ikacheze michuano maalum?

Pia anza kujiuliza, Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) wako wapi, wanafanya nini? Kwa nini wanaanzisha madudu haya na TFF kama viongozi wakuu wa soka nchini wako kimya!

Sakata limeanzia kwa uongozi wa TFF kukubali kuiruhusu Azam FC eti ikashiriki michuano maalum inayofanyika nchini Zambia ambako walialikwa na wangecheza na timu kama Zesco na TP Mazembe!

Azam FC wanaondoka vipi wakati ligi kuu inaendelea? Unaweza vipi kuahirisha ligi kwa ajili ya michuano maalum ambayo imeibuka tu kama uyoga?

Vipi hii TFF inashindwa kuona haya au kujisikia vibaya wadau wanavyolalamika kutokana na ratiba ya hovyo, isiyokuwa na mahesabu wala isiyolenga maendeleo ya ligi yenyewe na mpira nchini.

Kila baada ya mechi mbili, ligi inaahirishwa. Kila baada ya mechi tatu, ligi inasimama. TFF wanaona sawa na utaona Tanzania sasa inarudi kulee, ambako Fat ilikuwa ikifanya upuuzi kama huu.

Niliwahi kusema kwamba Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF amepewa nafasi kubwa na inayomzidi nguvu kiuwezo.

Nikatolea mfano wa kwamba, ni mtu anayaingia kwenye nafasi ambayo si saizi yake kwa maana ya rekodi ya utendaji wake.

Aliwahi kuwa bosi wa mashindano yapi, yalikuwaje, yalifanikiwa vipi? Nilisema kama yupo pale ni kishikaji tu. Sasa anaongoza ligi mbovu na ya hovyo kabisa na haijawahi kutokea kwa miaka yote ya mabadiliko tokea Fat ilipoanza kuitwa TFF.

TFF wanafanya hivyo kwa nini? Urafiki, kubebana? Au wanataka kumfurahisha nani hasa na kwa faida ipi? Lakini wataweza vipi kuwakataza Yanga nao wasiende kambini Afrika Kusini? Au Simba wasiende katika michuano ya kubuni ya Kenya?

Wanabuni kwa kuwa naona wanachezewa na watu wasiodhamini maslahi yao, wasiojua kama timu nyingine zinapoendelea kucheza na nyingine hazichezi ni ukwamishaji wa ratiba, pia kunaweza kusababisha hata upangaji wa matokeo mwishoni.

TFF hii imekuja kuivunja soka ya Tanzania na inaonekana haijali wala kuingia hofu. Kawaida anayehofia kutenda dhambi ni yule anayemuogopa Mungu.

Ninaamini TFF ingeweza kufanya mema kwa kuhofia kutenda upuuzi angalau kwa kuwaonea aibu wadau wa mpira waliowapa dhamana. Lakini hilo hawana, hivyo tuendelee kutegemea madudu huku TFF ikigeuzwa sehemu ya wasio na ujuzi, wasio na nia nzuri ya maendeleo kupumzikia.




1 COMMENTS:

  1. Kitendo cha kuchukua kiongozi wa Azam ndo awe mwenyekiti wa bodi na Azam wakadhamini ligi tayari ilishakuwa ni tatizo na hili nililiona wakati wa kusaini mkataba! TFF na Bodi walikuwa hawamsikilizi mtu yote ni kuhofia nguvu ya hela ya Azam. Hivi fikiri Nike ndo wangekuwa wanaimiliki RM au Barca halafu wenyewe ndo kiongozi ndo awe kiongozi wa Ligi ingekuwaje!?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic