February 28, 2016


Baada Francis Cheka kuibuka na ushindi dhidi ya Geard Ajetovic raia wa Serbia anayefanya kazi zake nchini Uingereza, nilimsikia Yasin Abdallah maarufu kama Ustaadhi akisema maneno mengi kujisifia.

Ustaadhi ambaye ni Rais wa TPBO, alianza kuzungumza akijigamba kwamba upande wa bondia wamekuwa wakiiwakilisha nchini vizuri.

Alianza kuwananga watu wa soka kuwa ni vichwa vya wenzawazimu huku akilia serikali imewatenga.

Kilichonishangaza ni kumuona kiongozi wa mchezo fulani, tena mwenye cheo cha rais akizungumza maneno ya kipuuzi kabisa ambayo kamwe hauwezi kutarajia kumsikia akifanya vile.

Swali, kiongozi anapaswa kupambana kuupigania mchezo husika au kulalama wengine wanapendelewa. 
Mara kadhaa, nimeona viongozi wengi wasio na ufundi wa kutosha na mchezo wakitoa kauli kama hizo. Wako hata kwenye mpira wa kikapu, netiboli na mingineyo.

Wanataka kulazimisha mioyo ya watu kuachana na soka na kupenda michezo mingine. Ni jambo la kijinga kabisa na kupoteza muda.
Anayependa soka, anaweza kuperad ngumi na mpira wa kikapu. Anachoangalia ni burudani ya moyo wake. Anapofurahishwa ndipo anapokwenda na Ustaadhi anapaswa kujua kuwa wadhamini wanaangalia wapi watatangazika.

Pia wanaangalia sehemu ambayo hawawezi kupata aibu. Kwani mara ngapi wadhamini wamejitokeza, wakatoa fedha zao halafu siku ya pambano wakaambulia aibu kwa kuonekana mabondia wanadai fedha zao.

Ustaadhi hajui kwamba mabondia wetu ukizungumzia nje ya nchi wamekuwa wakidundwa mara kibao na wanatumika hovyo? Anajua wako mabondia wanadhulumiwa na fedha wanakula viongozi wa mashirikisho au mapromota na wenyewe wanapata kiduchu.

Kuna matatizo mengi sana kwenye ngumi, Ustaadhi angepazwa kuelekeza nguvu huko kuliko kuwa mtu wa kulialia au anayepayuka maneno yasiyokuwa na msingi.
Walakini ni mkubwa, kwenye mapambano ya ngumi mengi huwa na matatizo kibao. Aanze kushughulikia masuala kama hayo, mengine yatafuatia. 

Kama ana malalamiko, alitaka kuipelekea serikali, tayari amepata nafasi ya kukutana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, angeyasema huko.

Kama ni wadhamini, kwanza wawavutie watu. Wadhamini hufuata watu na si maneno mengi yasiyokuwa na sababu za msingi.

Lakini bado ninamkumbusha ustaadhi, kutaka kushindana na upenzi wa watu katika soka ni kupoteza muda. Hakuna aliyewahi kushika kipaza sauti akapita akiwaomba watu kuupenda mchezo huo wa masikini wengi.

Wamerekani na mpira wa kikapu, wamejaribu kupigana nao kuuangusha lakini imeshindikana. Nao sasa wana ligi maarufu ya mchezo wa soka.

Hivyo vizuri kufanya mipango bora ya muda mfupi na mrefu kwa ajili ya mchezo wa ngumi na si maneno mengi yasiyokuwa na tija.

Salamu kwako Ustaadhi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic