Na Saleh Ally
HAKUNA tofauti ya rais aliyepita wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter na yule wa sasa, Gianni Infantino kama utazungumzia suala la kipara, wote wawili wanavyo.
Kidogo unaweza kuwatofautisha kwa kuwa kipara cha Blatter angalau kulikuwa na upande wenye nywele kidogo lakini Infantino ameamua kunyoa nywele zote.
Ukiachana na upara, wawili hao wanafanana kwa mambo mengi, moja ukianza na utaifa, wote ni raia wa Uswisi, wako kwenye mpira siku nyingi na hata tofauti ya vijiji vyao ni umbali wa kilomita sita pekee. Infantino mwenye umri wa miaka 45, anatokea katika Kijiji cha Brig eneo la Valais, wakati Blatter kwao ni mji mdogo wa Visp.
Infantino amechaguliwa kwa kura 115 akimzidi mpinzani wake mkubwa Sheikh Salman bin Ebrahim al-Khalifa kura 27, hii inaonyesha kweli kulikuwa na ushindani mkubwa.
Infantino ameshinda uchaguzi huo wa Fifa siku chache baada ya kuonekana akiwa nchini Rwanda ambako alikwenda kufanya kampeni katika michuano ya Kombe la Chan iliyofanyika nchini humo.
Muda mwingi, Infantino alionekana kama mtu wa kawaida na alipenda sana kukaa karibu na waandishi wa habari.
Licha ya kwamba alipata nafasi ya kukutana na Rais Paul Kagame alipotembelea Ikulu ya Kigali, lakini aliendelea kujionyesha yeye ni mtu wa watu.
Baada ya ushindi wake, umeona namna baadhi ya nchi nyingi za Ulaya wakiwemo wanamichezo hasa wanasoka na viongozi walivyoandika ujumbe mitandaoni kumpongeza. Imekuwa nadra kuona watu kutoka Asia au Afrika wakifanya hivyo kwa wingi.
Vita kubwa iliyopo Fifa, inamfanya Infantino kuendelea kubaki katika kundi la “Walewale” na huenda sasa ukawa ni wakati wa Afrika kuyumba na hasa Afrika Mashariki ambako ni “kizazi” cha baa la njaa kwa maendeleo ya soka.
Infantino alikuwa Kigali kwa kuwa alijua nchi nyingi za Afrika Magharibi na Kaskazini zilizo na nguvu katika soka la Afrika zilikuwa nchini humo. Hata wakati wa kampeni, utaona walioshindwa ndiyo waliotembelea na kufanya kampeni Tanzania.
Nini ambacho Infantino anaweza kuisaidia Fifa kubadilika kwa kuwa anatoka chini ya bosi Michel Platini ambaye ameingia katika kashfa na mwisho kusimamishwa kama ilivyokuwa kwa Blatter ambaye ameisukuma Fifa kuwa moja ya shirikisho lenye nguvu lakini wahusika wake wana nguvu ya kuiba bila kuulizwa?
Angalia mfumo wa Blatter umesaidia hata viongozi wengi wa mashirikisho ya Afrika kuiba wanavyotaka na wakawa wakali kila wanapoulizwa hata na serikali.
Wanasema “za mwizi arobaini”. Mwisho Blatter kaondoka kwa aibu, lakini upande mmoja unaona amekosea na mwingine haikuwa hivyo.
Upande mmoja ni kweli Fifa kulikuwa na ubadhirifu wa juu kabisa. Upande wa pili, kitendo cha Kombe la Dunia kuchukuliwa na Urusi halafu Qatar, kimeonyesha kuwakera wakubwa kama Marekani, England, Ufaransa na wengine ambao wameonyesha misuli na mabavu yao, wakamng’oa .
Athari yake inakuja hivi, kweli Infantino ambaye ana uraia wa nchi mbili; Italia na Uswisi, ataweza kuwabana viongozi wa mashirikisho ya Afrika kutotumia fedha vibaya huku wakitumia mwamvuli wa Fifa? Pili ataweza kuitetea Afrika dhidi ya vigogo hao wanaoiona ina maana pale unapofikia wakati wa kuomba kura tu? Kwani hata Infantino ameonyesha anaipenda Afrika ulipofika wakati wa kura!
Kuingia kwa Infantino baada ya Blatter kwa mambo mengi inaonekana ni sawa na chupa mpya yenye mvinyo wa zamani. Kwani hata aliyekuwa akifanya kazi kwa karibu sana, Platini, naye ameingia kwenye mkumbo wa “wachafu”.
Wakati wa kampeni zake, Infantino aliahidi dola milioni 5 kwa kila shirikisho kati ya mashirikisho 209 ambayo ni wanachama wa Fifa. Akaahidi dola milioni 40 kwa kila shirikisho la bara kama Caf na dola milioni 4 kwa kila michuano ya vijana kwa kanda, maana yake hapa kama atakuwa mkweli, michuano ya vijana ya Afrika itaboreka zaidi.
Unarudi palepale kwamba kiongozi huyo wa zamani wa Uefa, amewavutia wengine kutokana na ahadi kubwa ya fedha na hilo ndilo lilimfanya Blatter abaki madarakani tangu mwaka 1998.
Viongozi wengi wa mashirikisho pia huangalia maslahi yao binafsi. Mikutano ya Fifa, mingi ilitawaliwa na rushwa, fedha zikagawiwa kwa wajumbe, jiulize Infantino kama anahitaji wapiga kura atalikwepa hilo?
Ndiyo maana nasema, pamoja na sifa bora ya uchapakazi ya Infantino ambaye ni mwanasheria kitaaluma, bado inaonekana Afrika atakuja baadaye baada ya kuwaridhisha “wakubwa”.
Blatter alipoanza, pia ilikuwa hivyo, Afrika akaanza kuingia na kujitanua baada ya kuona anabanwa zaidi Ulaya. Akatafuta nguvu kubwa ya kura Afrika. Kwa Infantino, sasa bado ana nguvu kubwa Ulaya, huenda asiwe na sababu ya kulalia Afrika au Asia na badala yake nguvu ikaendelea kubaki Ulaya na Marekani kwa wakubwa na mabara mengine yakawa “bendera fuata upepo”.
Tanzania ipambane kivyake, kamwe isije ikatokea kiongozi wa TFF akatuambia tutafaidika na ujio wa Infantino. Badala yake kama ni ubora wa mabadiliko, ufanywe kwa dhati na Watanzania wenyewe, Fifa watatukuta mbele.
Hadi sasa, kama Mwafrika sioni chochote cha kumfurahia ndugu huyo wa Blatter. Wakati mwingine nasema bora angebaki Blatter ambaye hata kama alijifaidisha, basi na Afrika nayo ikafaidika.
Dalili za Afrika kusubiri zimeanza kuonekana mapema. Rais wa TFF, Jamal Malinzi angalau aliambulia picha ya pamoja na Infantino, lakini hatuna uhakika kama alikumbuka kumueleza matatizo yetu na kweli atakuwa tayari kuyafanyia kazi.
Lakini bado hajawa wazi huyo Infantino kama atakuwa na sera ya kuwalinda “majizi” kwa mgongo wa Fifa au atapambana nao ili maendeleo ya dhati yapatikane.
Tanzania haina sababu hata nusu ya kushangilia mabadiliko ya Fifa kwa kuwa yanaonekana wazi ni kwa manufaa ya wachache wenye nguvu. Acha wabadilishane, vema sisi tutakomaa kivyetu huku wenyewe wakiendelea kuunywa mvinyo wao wa zamani kwenye chupa mpya.
MARAIS WA FIFA:
1904-06: Robert Guerin (Ufaransa)
1906-18: Daniel Woolfall (England)
1918-21: Hakuchaguliwa rais mpya baada ya kifo cha Woolfall
1921-54: Jules Rimet (Ufaransa)
1954-55: Rodolphe Seeldrayer (Ubelgiji)
1955-61: Arthur Drewry (England)
1961-74: Sir Stanley Rous (England)
1974-98: Joao Havelange (Brazil)
1998-2015: Sepp Blatter (Switzerland)
2016-: Gianni Infantino (Switzerland)
0 COMMENTS:
Post a Comment