February 15, 2016



Na Saleh Ally
MAJIMAJI ya Songea sasa iko katika nafasi ya 14 katika Ligi Kuu Bara, jumla ya timu zinazoshiriki ni 16.
Timu hiyo kutokea mkoani Ruvuma, ndiyo imerejea katika ligi hiyo msimu huu. Kwa mtazamo wa sasa ni timu ya kawaida kabisa, lakini unaujua ukubwa wake.

Kati ya timu chache zenye majina makubwa unapozungumzia soka ya Tanzania. Ilishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mara tatu 1986, 1989 na 1998. Ikiwa ni baada ya kubeba ubingwa wa Muungano.

Majimaji ilikuwa timu ya kwanza ya mikoani kuwanunua wachezaji nyota kabisa wakati huo kama Abdallah Kibadeni ‘King Mputa’ akitokea Simba kama ilivyokuwa kwa Madaraka Selemani, pia Peter Tino aliyetokea Pan African.

Lakini ilikuwa na wachezaji tegemeo na gumzo hadi katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kama Selestine Sikinde ‘Mbunga’, Octavian Mrope na wengine wengi. Lakini si Majimaji ya sasa.

Ukubwa wa Majimaji iliyoanzishwa katika miaka ya mwishoni ya 1970 katika mikono ya Mkuu wa Mkoa, Lawrence Gama, ulitokana na uzalendo wa Wanaruvuma pamoja na bosi huyo wa mkoa.

Gama ndiye aliyeanzisha mfumo wa kuichangia Majimaji kwa kila aliyekuwa ananunua bidhaa. Iliongezeka shilingi moja ambayo moja kwa moja iliingia katika kuichangia timu hiyo.

Fedha hizo ziliifanya Majimaji kuwa na nguvu kubwa, ikawa na uwezo hata wa kuwanunua wachezaji hao nyota na mwisho ikawa kubwa na hata kutikisa Tanzania Bara na Visiwani. Baadaye ikacheza michuano mikubwa ya Afrika.
Bado wapo wanaokumbuka historia ya yule kiongozi aliyelazimika kuonyesha mapenzi ya dhati kwa Yanga. 
Songea akaonekana ni msaliti, akatengwa na mwisho akahamia Njombe.

Pamoja na uchangiaji, uongozi bora wa Gama, lakini wana Ruvuma walionyesha uzalendo na mapenzi ya dhati kwa timu hiyo kiasi cha kuungana kujenga Uwanja wa Majimaji.
Uwanja wa Majimaji ulijengwa chini ya Azimio la Mlale ambalo ni mtoto wa Azimio la Arusha. Hakika kwa anayejua, uwanja huo ulijengwa kwa nguvu za wananchi.

Wako waliotoa fedha, wako waliojitolea kufyatua matofali na kujenga. Wanafunzi walifanya kazi ya kubabe maji kwa ajili ya ujenzi na Majimaji ikaanza kucheza kwenye Uwanja wa Majimaji.

Kuondoka kwa Gama alipohamishiwa mkoani Tabora ambako aliianzisha Mirambo, ulikuwa ni mwanzo wa kuanza kuteleza kwa Majimaji ambayo sasa ni timu ya kawaida kabisa na mapenzi ya Wanaruvuma si yale yaliyozoeleka.

Leo Majimaji haina nguvu kisoka licha ya kupata Sh milioni 100 kutoka Azam TV pamoja na udhamini wa Symbion. Inaonekana ni timu ya kawaida kwa kuwa walioizunguka kuanzia viongozi, wachezaji na mashabiki na wanachama, hawajui faida ya mapenzi.

Mambo haya matatu ni tatizo kubwa kwa Ruvuma, Songea na Majimaji yenyewe. Kwanza ni uongozi mbovu, wengi wao si wabunifu, hakuna aliyetayari kuiga hata nusu ya ubunifu wa Gama alioufanya zaidi ya miaka 20 iliyopita. Waliopo sasa wanaishia kufikiria na hakuna kubwa wanaloweza kufanya.

Pili; wanachama na  mashabiki, hawako tayari kuchangia zaidi ya kutaka mafanikio. Tena wakiwa wamekaa kando wanalaumu tu, huku wakifananisha na Majimaji ya enzi hizo.

Tatu; kuna watu, wanachama au mashabiki, pia viongozi. Wako ndani ya Majimaji kwa ajili ya faida zao binafsi hasa kisiasa na kuisaidia klabu hiyo kongwe ambayo inastahili kufanya vizuri kwa kuwa imehangaika sana kurejea Ligi Kuu Bara.

Majimaji sasa haina uhakika wa kubeba ubingwa, lakini haina uhakika wa kubaki Ligi Kuu Bara. Ukitulia, utanijibu, sasa iko Ligi Kuu Bara wapi na inafanya nini?

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic