Bosi wa Simba katika benchi la ufundi, Jackson Mayanja, ametamba kuwa anasubiri ushindi mmoja tu katika mchezo ujao dhidi ya Yanga ili aweze kuamini kuwa wana asilimia kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Baada ya ushindi wa juzi dhidi ya Stand United ugenini, Mayanja ya Simba imeshinda mechi zote saba ilizocheza, ikiwemo ya Kombe la FA dhidi ya Burkina Faso.
Mayanja amesema mchezo ujao dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga, ndiyo utamfanya atangaze ubingwa.
“Kwanza yote kwa yote namshukuru Mungu kuniwezesha kupata matokeo mazuri tangu nijiunge na Simba na hii inatokana na ushirikiano mzuri ninaoupata kutoka kwa viongozi wangu pamoja na wachezaji kufuata maelekezo ninayowapa katika mazoezi ambayo yanawasaidia kucheza soka la kuvutia na kupata matokeo mazuri.
“Katika mechi zilizobaki, mechi ngumu zaidi itakuwa ni dhidi ya Yanga ambayo naamini kama tutashinda, basi nitatangaza nafasi ya ubingwa, kwa kuwa tukishaiacha Yanga pointi nyingi, tunakuwa katika nafasi nzuri zaidi,” alisema Mayanja.
Simba itacheza na Yanga Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwa mbele yao kwa tofauti ya pointi mbili huku Yanga ikiwa na mchezo mmoja mkononi.
0 COMMENTS:
Post a Comment