Na Saleh Ally
MWANADAMU mwenye afya njema hukapua macho yake takriban mara milioni 4.2 kwa mwaka.
Si rahisi hata kidogo mwanadamu kujua kuhusiana na hesabu hizo au kuamini anaweza kufikisha idadi hiyo ya kukapua bila ya kuchukua uamuzi mgumu wa kufanya uchunguzi wa kina.
Leicester City, sasa inaongoza Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi tano. Mkononi imebakiza mechi 13 kama ilivyo kwa wengine ili kupata uhakika kama inaweza kuwa ndiyo wafalme wapya.
Wafalme wa sasa ni Chelsea, tayari hawamo kwenye mbio za kuweza kulitetea taji, angalau Arsenal, Tottenham, Man City na Manchester United. Hawa wanne wanaweza kumfukuza Leicester City.
Leicester, timu iliyopanda daraja na kuonekana kama ilikuwa nguvu ya soda tu, tayari imebakiza dakika 1,170 kuweza kuwa na uhakika wa kuwa bingwa. Kikubwa inatakiwa kucheza vizuri karata zake.
Inaweza kufanya hivyo kwa kuwa tayari imecheza karata yake vizuri dakika 2,250 hadi sasa na imeweza kutofautiana na aliye katika nafasi ya pili kwa pointi tano. Kweli, hata kama ligi iko ukingoni itashindwa kucheza vizuri karata za dakika 1,170?
Ukiangalia mechi 13 zilizobaki ndani yake, kuna vigogo wanne ambao italazimika kumalizana nao ambao ni Arsenal (mechi inayofuata), Manchester United na Chelsea.
Pamoja na hivyo, Leicester ina nafasi ya kumaliza presha mapema kwa kuwa mechi ya Everton itakuwa ni ya pili kutoka mwisho, Chelsea itakuwa ni ya kufunga ligi. Kama itafanya vema, huenda mechi hizo zikawa ni za kufunga dimba tu baada ya kuwa imeishabeba ubingwa.
Zile hisia za Leicester ni nguvu ya soda, zimetoweka. Hii ni baada ya kuitwanga Manchester City kwa mabao 3-1 ikiwa nyumbani kwake Etihad. Timu inayoiangusha City kwa kipigo hicho, maana yake ina uwezo wa kuifunga timu yoyote.
Hali ya kujiamini kwa Leicester imepanda kwa kiasi kikubwa na iko katika hesabu ya timu kubwa za Ligi Kuu England kwa msimu wa 2015-16.
Awali, Kocha Mkuu, Claudio Ranieri alionekana ni mkubwa sana, wako waliomshangaa kurejea England na kuamua kuifundisha Leicester wakati alionekana ni kocha saizi ya Manchester United, Chelsea au Arsenal.
Sasa tayari timu imekuwa kubwa, ameifanya kufikia ukubwa huo wa timu nyingine ambazo zilionekana ndiyo alipaswa kuzifundisha.
Kupoteza:
Kingine kinachofanya Leicester ionekane inaweza ni mechi ilizopoteza. Katika mechi 25 ilizocheza, imepoteza mechi 2 tu na kuwa timu iliyopoteza mechi chache zaidi.
Vigogo kama Man City na Man United, zimepoteza mara 6, hii ni mara tatu ya Leicester. Liverpool imepoteza mara 8 na Chelsea ambao ni mabingwa watetezi wamepoteza mara 9.
Kufunga:
Kingine ambacho kinaweza kuwa kigezo cha kuwawezesha kutwaa ubingwa. Ni uwezo wa kufunga mabao, hadi sasa wametikisa nyavu mara 47 na ndiyo timu iliyofunga mabao mengi zaidi hadi sasa, sawa na Man City.
Wanaowafuatia angalau ni Tottenham wenye mabao 46, Everton wana 45, Chelsea wana mabao 32 na Man United wanaangukia pua na mabao 31 tu.
Hii ni sehemu nyingine inayoonyesha wanaweza kufanya kinachoaminika hakiwezekani kupitia dakika 1,170 walizobakiza.
Difensi:
Kidogo hapa ndiyo wanapaswa kuwa makini zaidi. Safu yao ya ulinzi si ile ngumu ya kutisha na huenda kiungo bora na wafungaji hatari wanapunguza presha kubwa kwenye safu ya ulinzi.
Leicester imefungwa mabao 27, si timu iliyofungwa mabao machache zaidi.
Spurs imefungwa mabao 19 tu, ndiyo yenye safu ngumu zaidi hadi sasa. Inafuatiwa na Man United iliyofungwa 21, Arsenal wamefungwa mabao 22, Southampton mabao 24 na Man City wameruhusu 26.
Lazima Ranieri aende na staili anayoiamini ili kupunguza presha kwenye safu ya ulinzi. Kama mfumo wake utakwama kidogo, inaonekana safu ya ulinzi inaweza kuruhusu mabao, jambo ambalo ni hatari.
Mwenendo:
Kingine kinachoonyesha wanaweza kuwa mabingwa ni mwenendo wao sasa. Katika mechi sita zilizopita katika timu zote za Ligi Kuu England, Leicester ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza mchezo. Katika mechi sita imeshinda minne na sare mbili.
Inafuatiwa kwa ubora na Spurs, imeshinda minne, sare moja na kupoteza mmoja, Man City, sare mbili, imepoteza mmoja na kushinda mitatu.
Ubora half time:
Ubora wa hadi mapumziko wa Leicester uko juu. Kwani mechi nyingi hadi mapumziko ilikuwa inaongoza. Hivyo kupata wastani wa 36%. Imekuwa sare na timu pinzani hadi mapumziko kwa wastani wa 40% na mechi ambazo ilifungwa hadi kufikia mapumziko ni wastani wa 24%.
Hesabu bora kisoka, kocha na wachezaji hutakiwa kuugawa mchezo mara mbili na kuzicheza dakika 45 za kwanza, halafu wanajipanga kuzicheza za pili ambazo mara nyingi unakuwa umeishajua mbinu nyingi za mpinzani.
Dakika 45 za kwanza ni muhimu zaidi kwa maana ya kumsoma mpinzani na ikiwezekana kummaliza. Leicester wako vizuri katika hilo.
Vardy & Mahrez:
Lazima Leicester wasali hawa jamaa wasiumie. Ni watu muhimu sana na wana mambo mawili mazuri na makubwa yanayopishana.
Jarmie Vardy kafunga mabao 18, Riyad Mahrez amefunga 14, jumla ni 32, si mabao machache.
Raha zaidi kila mmoja ana ubora wa aina yake. Katika mabao 18, Vardy 11 amefunga nyumbani na 7 ugenini.
Mahrez amefunga 14, kati ya hayo 10 ni ugenini na 4 tu ndiyo nyumbani. Hivyo, hawa jamaa wana watu wa kufanya kazi bila ya kubabaisha wanapokuwa nyumbani au ugenini. Wako kamili.
Nyumbani & ugenini:
Hiki pia ni sehemu ya kuonyesha wanaweza kuwa mabingwa. Nyumbani wamecheza mechi 12 na kukusanya pointi 25, wanashika nafasi ya pili baada ya Man United iliyokusanya pointi 28 baada ya mechi 13 nyumbani. Leicester ndiyo wanaongoza kwa kukusanya pointi nyingi ugenini.
Wamecheza mechi 13 na kukusanya pointi 28. Kama timu ina uwezo wa kuchukua pointi nyingi zaidi ugenini, nini kitawazuia kuwa mabingwa?
MSIMAMO, LEICESTER ILIVYOPAMBANA MARA 25
Nyumbani Ugenini
1. Leicester City
2. Tottenham 1-1 0 - 1
3. Manchester City 0-0 1 - 3
4. Arsenal 2-5 14 Feb
5. Manchester Utd 1-1 30 Apr
6. West Ham Utd 16 Apr 1 - 2
7. Southampton 2 Apr 2 - 2
8. Everton 7 Mei 2 - 3
9. Liverpool 2-0 1 - 0
10. Watford 2-1 5 Mar
11. Stoke City 3-0 2 - 2
12. Crystal Palace 1-0 19 Mar
13. Chelsea 2-1 15 Mei
14. West Bromwich 1 Mar 2 - 3
15. Bournemouth 0-0 1 - 1
16. Swansea City 23 Apr 0 - 3
17. Newcastle Utd 14 Mar 0 - 3
18. Norwich City 27 Feb 1 - 2
19. Sunderland 4-2 9 Apr
20. Aston Villa 3-2 1 – 1
0 COMMENTS:
Post a Comment