February 10, 2016

ZANZIBAR HEROES
Na Saleh Ally
UJINGA unaoendelea Zanzibar kupitia watu wachache kabisa wanaoangalia nafsi na furaha za mioyo yao, unazidi kuliteketeza soka la kisiwa hicho, sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuna mgogoro mkubwa, Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Ravia Idarous Faina, amesimamishwa. Tayari mahakamani kuna kesi, Shirikisho la Soka Afrika (Caf) limekemea na kutaka suala hilo limalizwe.

Kila utakaposikia kuhusiana na soka Zanzibar, asilimia 80 itakuwa inahusisha migogoro na haiishi na utaona wahusika wanajivunia kuendelea kwa migogoro hiyo.

Kumekuwa na juhudi kuhakikisha kesi hiyo inafutwa lakini bado inaonekana kuna wale wasiotaka iishe, hii inaonyesha wazi ni maslahi binafsi ambayo yanaweza kuwa ya nafsi au kujiendeleza kutaka kujinufaisha.

Kikubwa ambacho kinaonekana wazi ni hiki, ndoto ya maendeleo ya soka Zanzibar sasa itabaki kuwa hadithi hadi wale wanaolumbana kwa faida yao binafsi waamue kukionea huruma kizazi cha soka Zanzibar.
Nani leo anaweza kumuona tena mtu mfano wa Abdul Malaika, mshambuliaji wa Malindi, aliyekuwa tishio, aliyekuwa akiogopwa Zanzibar, Tanzania Bara hata Afrika kote?

MAFUNZO
Wachezaji kama Amour Aziz, Ali Kibichwa, Victor Bambo waliong’ara na Malindi.

Lakini ni vigumu tena kusikia makali ya timu za Zanzibar kama ilivyokuwa kwa akina Small Simba, Miembeni, Malindi na Yanga na Simba walijiandaa wakijua wanakwenda kukutana na wanaume kazini. Lakini kwa sasa, Simba, Yanga, Mtibwa, Azam FC hata zinapokwenda kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, zinajua zinakwenda kujipigia tu timu za Zanzibar.  Imefikia sasa, inaonekana ni ajabu kwa timu ya Bara kufungwa na timu ya visiwani!

Wafadhili kama yule Naushad Mohammed, nani anaweza kujitokeza tena? Hali ilivyo sasa ni migogoro mitupu. Hakuna timu ya Zanzibar inayoweza kununua tena mchezaji nyota kama ambavyo kina Edibily Lunyamila, Nico Bambaga, Athanas Michael walinunuliwa kutoka Yanga au Simba na kwenda kucheza Zanzibar tena katika kipindi wanachong’ara.

Siku hizi, mchezaji wa Zanzibar ili aonekane kwenye ulimwengu wa soka, lazima anunuliwe Tanzania Bara. La sivyo atabaki kuwa hadithi!

Achana na wanaotoka Bara, timu za Zanzibar kama Malindi zilinunua wachezaji hadi kutoka kwingine Afrika kama Moldon Malitoli kutoka Zambia, pia Ulaya, mtu kama Julian Albertov kutoka Bulgaria.

ZANZIBAR HEROES
Hakuna anayeweza kudhubutu kufanya hivyo kwa kuwa mpira unanuka na kufanana sura, umbo hadi kutembea na migogoro isiyokuwa na sababu na hakuna anayeweza kubisha kwamba wanaosababisha migogoro hiyo ya kipuuzi na isiyo na faida ni Wazanzibar wenyewe.

Hapa ndiyo unabaki unajiuliza, hivi hawa, nikimaanisha wote wanaosigana na kulumbana kwa sauti kila kukicha hawana watoto, hawana wajukuu, hawasikii maumivu katika mioyo yao namna Zanzibar inavyoangamia na miaka inakwenda?

Inafikia wakati ninajiuliza, hivi kweli watu wale ni Wazanzibar, kama ni hivyo vipi wana uchungu wa hisia zao binafsi kuliko hisia za utaifa ambao unawahusu watu wengi na sasa imebaki kwa faida yao!

Huu ndiyo wakati mwafaka, wapatane ili kumaliza mgogoro ili Zanzibar irejee. Kama hawawezi vizuri pande zote mbili ziondoke kwenye soka la Zanzibar na wanaweza kufanya mambo yao mengine na kuna kazi nyingi, si lazima soka kwa kuwa mimi ninaamini, bila wao, mpira wa Zanzibar utaendelea zaidi. Waondoke, tafadhali, ondokeni zenu, mnaikwamisha Zanzibar.

Angalia leo, Zanzibar inadhaminiwa na Grand Malt. Hawa jamaa ni jasiri kabisa kwa kuwa utaona ligi haina manufaa tena, huenda wameamua kujitolea.

Kwa kuwa wafadhili wamekuwa kama wahisani, kwa mwaka timu inapewa Sh milioni 8 tu! Mzunguko wa kwanza Sh milioni 4 na wa pili hivyohivyo. Fedha hizo zinaweza kutumiwa na timu ya Tanzania Bara kwa siku mbili au tatu. 


Vipi sasa ligi ya Zanzibar itatoa matunda makubwa?
Tunajua Zanzibar kuna vipaji, tena vingi sana na kuna mifano tumeona ambayo ni hai. Lakini wanaolumbana ndiyo tatizo na mwisho wasimtupie mzigo mtu mwingine.

Kikubwa ni hivi; mpatane, kama hamuwezi wote ondokeni, waachieni Wazanzibar wanaotaka maendeleo, waongoze mpira wao, nyie kaanzisheni Chama cha Migogoro ya Soka Zanzibar (Chamisoza), muendeleze malumbano yetu yasiyo na tija wala hisia za dhati za maendeleo, mimi nimewachoka kabisa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic