KIIZA VS BOSSOU... |
Na Saleh Ally
UNAWEZA kusema mechi ya watani wa jadi inaweza kuwa sehemu ya majibu ya ubora wa kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania.
Kwamba inakutanisha timu kubwa kabisa za Tanzania. Maana yake unategemea kuwa na wachezaji mahiri angalau sita au saba ambao watakuwa tegemeo hasa katika timu ya taifa.
Ukongwe wa Simba na Yanga, unawapa nafasi ya kuingia kwenye msukumo wa kusajili wachezaji bora ambao wanakuwa tegemeo katika timu ya taifa.
Utegemezi wao katika kikosi cha Taifa Stars lazima uanzie katika klabu zao. Lakini hakuna ubishi, mechi ya Jumamosi kati ya Yanga na Simba inaonyesha bado tuna safari ndefu.
Kama kweli Yanga na Simba ndiyo kipimo, basi safari ni ndefu kwa kuwa ilionekana wazi waliokuwa wenye mechi hiyo ni wachezaji wa kigeni.
Wachezaji wa nyumbani ni wachache mno walioonyesha kiwango bora na kuwa tegemeo hasa katika mechi hiyo. Huku ikionekana hata utegemezi wa kikosi katika karibu kila sehemu nyeti ilikuwa na wageni na ndiyo walioibeba mechi hiyo.
KAZIMOTO VS JUMA ABDUL, BOSSOU |
Kikosi cha Yanga chini ya Kocha Mholanzi, Hans van Der Pluijm kilianza na wageni sita, Watanzania walikuwa watano. Mganda Jackson Mayanja wa Simba akaanza na wageni wanne na Watanzania sita.
Kwanza nikukumbushe, kikosi kilichoanza na wageni wengi ndicho kilichoibuka na ushindi. Pia wageni wakaonyesha uwezo wa juu zaidi.
Mfano katika lango, kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’, hauwezi kumsifia hata kidogo kwa kuwa hakupata kashkash za kutosha kutokana na kudorora kwa safu ya ushambulizi ya Simba. Lakini Vincent Agbani, raia wa Ivory Coast alionyesha uwezo licha ya kufungwa mabao mawili ya kizembe kutokana na uzembe wa “kutupwa” wa mabeki wake.
TAMBWE, JUMA ABDUL NA MSUVA |
Katika safu za ulinzi, wageni Mbuyu Twite (Rwanda) na Vincent Bossou (Togo) ndiyo wakaonekana kufanya vizuri zaidi huku safu ya ulinzi iliyoongozwa na mzalendo Abdi Banda na Juuko Murshid wa Uganda ikidorora.
Katika wageni waliocheza hovyo au kiwango cha chini siku hiyo ni kiungo wa Simba, Justice Majabvi wa Zimbabwe, ambaye mara nyingi amekuwa ni mchezaji wa kawaida, lakini mechi hiyo ilimshinda kama ilivyokuwa kwa Juuko ambaye si kawaida yake.
Kwa upande wa kiungo ukizungumzia ulinzi na ushambulizi. Utaona Thabani Kamusoko (Zimbabwe) na Haruna Niyonzima (Rwanda) walifanya vizuri. Lakini hapa ndiyo sehemu pekee walipopata upinzani mkubwa kutoka kwa Jonas Mkude.
Mkude ndiye alionyesha kiwango cha juu zaidi licha ya kiungo cha Simba kuvurugika baada ya kutolewa kwa Banda. Alionyesha ni msaada na uwezo binafsi na huenda alikuwa mfano kwa wageni wengi.
Kwa upande wa washambuliaji, Donald Ngoma (Zimbabwe) na Amissi Tambwe (Burundi) ndiyo walikuwa wanastahili kupewa nafasi ya nyota wa mchezo.
AJIB VS JUMA NA KAMUSOKO |
Walijiamini, walifanya wanavyotaka na wakaweza kufunga na kuizamisha Simba kwa mabao 2-0 kila mmoja akifunga bao moja.
Mshambulizi yupi wa Tanzania alikuwa msumbufu au kivutio siku hiyo uwanjani? Kwamba alionekana ni hatari na siku akiwa ndani ya kikosi cha Taifa Stars atakuwa msaada kwa kikosi hicho? Jibu ni hakuna.
Tena unaweza ukatafuta upande wa Yanga na Simba pia. Lakini hata kwa viungo ukiacha alivyocheza Mkude siku hiyo hakuna pia.
Utaona kuna nafuu kidogo kwa upande wa walinzi wa pembeni. Utaona kulia Juma Abdul wa Yanga na kushoto Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba au Haji Mwinyi (Yanga) unaweza kusema ni hazina.
Sasa Stars itakwenda na wachezaji bora wa ulinzi pekee? Unaweza kusema Stars haichaguliwi kwa Yanga na Simba pekee. Lakini angalia kwingine, Azam FC, Mtibwa Sugar, Prisons, Majimaji na nyingine. Halafu angalia wangapi ni washambulizi bora na wana mabao mangapi katika msimamo wa wafungaji.
Sasa ni vita ya wageni tu katika ufungaji. Tambwe, Kiiza, Ngoma na Watanzania wanakuja baadaye. Unaweza kusema hata mechi kubwa ya Tanzania ni kwa msaada ya watu wa Zimbabwe, Burundi, Rwanda na Uganda.
KESSY VS MSUVA |
Wala asitokee mtu akasema vipi England kuna Chelsea, Arsenal na nyingine na hazina washambulizi hatari Waingereza. Hili nao linawasumbua sasa kwa kuwa hawakulitilia maanani kabla. Huu ndiyo wakati mwafaka kwetu kabla hatujachelewa.
YANGA |
Huu ndiyo wakati wa kujipima. Tanzania ina wachezaji zaidi ya wachezaji wanaocheza nje. Hivyo lazima iwe nao bora wanaocheza nyumbani ili wapate nafasi ya kuongeza idadi ya wanaocheza nje na kutengeneza Taifa Stars bora. La sivyo, hadithi ya ilibaki kidogo, haitaisha milele.
SIMBA |
0 COMMENTS:
Post a Comment