Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza kuwa Machi 20, mwaka huu ndiyo siku ya kutolea uamuzi juu ya hatma ya timu itakayopanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao kutoka Kundi C.
Timu za Polisi Tabora na Geita Gold Sports ndizo zinasubiri hatma hiyo baada ya kumaliza mechi zake zote zikiwa na pointi 30, huku TFF ikiwa na mashaka juu ya matokeo ya mwisho ya mechi zao ambapo Geita iliifunga JKT Kanembwa mabao 8-0, huku Polisi Tabora ikiikandamiza JKT Oljoro mabao 7-0 na kudai kwamba kuna mchezo mchafu wa upangaji matokeo ulifanyika, kitendo ambacho hakikubaliki kwenye soka.
Akizungumza na waandishi wa habari, Rais wa TFF, Jamal Malinzi, amesema kutokana na uzito wa ishu hiyo, walilazimika kuipeleka kesi hiyo katika kamati ya nidhamu ya shirikisho hilo ili kutoa hukumu kwa haki na usawa.
“Najua wengi wanataka kufahamu ni lini utapatikana mustakabali wa timu iliyopanda daraja kutoka Kundi C, niwaambie tu kesi hiyo itasikilizwa Machi 20, mwaka huu baada ya kufika kwenye kamati ya nidhamu ambayo ndiyo wenye jukumu la kusimamia ishu hiyo nzima.
“Kulikuwa kuna kila dalili za upangwaji matokeo na hukumu ya aliyetenda kosa hilo iko wazi, kama si kifungo cha maisha cha soka basi ni timu inashushwa daraja, lakini kutokana na kanuni za mashindano za Ligi Daraja la Kwanza kutokuwa na kipengele kinachotoa adhabu hizo, ndiyo maana tukaihamishia katika kamati ya nidhamu, baada ya hukumu kutolewa na kama upande mmoja hautaridhika basi unaruhusiwa kukata rufaa,” alisema Malinzi.
Malinzi aliongeza kuwa, hawakuweza kutoa hukumu mapema kutokana na uzito wa jambo hilo lililohitaji uchunguzi wa kina kwani kutokana na mchezo wa soka kuwa ni ‘fair play’, kuna uwezekano kwa timu zote zilicheza ‘fair play’ na kufungwa kihalali, ndiyo maana wanasubiri uchunguzi ufanyike kwanza kabla ya yote.
0 COMMENTS:
Post a Comment