March 19, 2016


 Na Saleh Ally
 HUU ni mwendelezo wa makala ya jana kuhusiana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Yanga, Jerry Muro.

Jana tuliishia Muro alipokuwa akizungumzia kuhusiana na walivyofarakana na Haji Manara ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji Mkuu wa Simba.

Muro alieleza kwamba aliwahi kumkopesha Manara Sh 100,000. Alipoanza kumdai ikawa mbinde hadi pale aliposhitaki kwa Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ambaye alimlipia.

Raha zaidi ni kwamba, Manara naye alitafutwa kuzungumzia hilo ambalo Muro amelisema.

SALEHJEMBE: Sasa ugomvi ukatokea wapi sasa, huenda ulidai kwa nguvu?
Muro: Mambo yalizidi kuwa magumu, ilifikia hadi Kaburu akaingilia baada ya kumueleza. Lakini ni mimi ndiye nilimwambia baada ya kuona mambo hayaeleweki.

SALEHJEMBE: Ok, sasa ikawaje?
Muro: Nikamueleza Kaburu, naye akamuita Haji pale, basi Kaburu akatoa fedha, akahesabu “tap tap tap” hadi ikafika laki akamlipia Haji.

SALEHJEMBE: Sasa kama ulilipwa Muro, kuna haja gani ya kuendelea kuonyesha hamuelewani?
Muro: Haji ndiye alinuna, lakini mimi sina tatizo naye, pia ni rafiki yangu kabisa.

SALEHJEMBE:Mmekuwa mkiwasiliana?
Muro: Inatokea na hii naona ana hasira kwa kuwa Yanga imeifunga Simba mara mbili, ingekuwa nao wametufunga katika mechi ya pili, ungeona hakuna hasira hata kidogo kutoka kwao.

SALEHJEMBE: Kwao kina nani?
Muro: Unawajua ndugu yangu, sema unataka niseme mengine.

Muro.

SALEHJEMBE:
 Uko huru, sema tu.
Muro: Hapana, ila nakuhakikishia sina matatizo na Haji. Tena nakumbuka baada ya kuwafunga mechi ya pili, tulikutana pale Uwanja wa Taifa, akaniambia siyo ndiyo niseme sanaa, kushinda siyo ishu kuuubwa. Nikamwambia nitasema, maana ndiyo kazi yangu.

SALEHJEMBE: Shida yako maneno yako ya shombo, sasa yanaelekea kuwa umetukana, Simba wanalalama sana, huoni si jambo jema?
Muro: Kama si jema, kila mmoja aseme nimetukana wapi. Hata Haji amewahi kuitukana Yanga.

SALEHJEMBE: Wapi, ilikuwaje?
Muro: Nimemsikia redioni akisema Yanga ni Mwali Kigego. Maana ya hili neno la Kizaramo, ni mwali ambaye ameolewa akiwa ameanza mapenzi. Sasa hili si tusi?

SALEHJEMBE: Mimi sijui Lugha ya Kizaramo.
Muro: Basi tafuta Mzaramo atakueleze kuhusiana na hilo.

SALEHJEMBE: Nilisikia uliwahi kumuita kiongozi wa Simba sanamu la Michelin, huoni si weledi wala si sahihi hata tukizungumzia umri tu?
Muro: Alianza mwenyewe, kazi yangu ni usemaji na mtu akiisema Yanga vibaya, basi lazima nijibu. Wakati wa kujibu napita njia zote.


SALEHJEMBE: Umejisifia wewe ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Yanga mwenye mafanikio zaidi, kivipi?
Muro: Kwanza mimi ni msomi, lakini nimechukua ubingwa, ngao ya jamii, sasa Yanga inasonga kimataifa. Hauoni ni mafanikio hayo? Sasa muulize na mwenzangu.

SALEHJEMBE: Mwenzako yupi?
Muro: Unamjua sana, usijikaushe!

SALEHJEMBE: Ila acha nikuulize Muro, wewe ni Mchagga kiasili. Lakini una maneno mengi hata kuliko watu wa Pwani, umejifunzia wapi?
Muro: (Kicheko), Ndugu yangu hii ni inborn spirit (asili). Mimi ni mtu wa kujituma. Nilikuwa ITV nikafanya yangu, nilienda TBC nikaonyesha. Wakati nakuja kwenye michezo watu wakahoji kama nitaweza. Si unaona mwenyewe, nikiingia kazini, naingia kweli. Mimi ni msemaji, nasema kweli. 

MANARA:
Baada ya hapo, juhudi za kumpata Manara zikafanikiwa ili aweze kujibu zile hoja za Muro. Hasa ile kuhusiana na deni, lakini pia suala la urafiki wao na baadaye kutokuwa wakizungumza.

SALEHJEMBE: Haji ulikopwa na Muro, ikawa mbinde kulipa hadi Kaburu akaamua kulipa, vipi yakhe?
Manara: Jerry anafanya makusudi ili niseme kitu halafu TFF waseme nimekosea watufungie wote. Maana ishu yake imewekwa kando kiaina. Kuwa mkweli hata wewe, nawezaje kwenda kumkopa Jerry?


SALEHJEMBE: Si ni rafiki yako, kwani kuna ubaya?
Manara: Sina urafiki na Muro, tunajuana kwa kuwa wote tuko kwenye uandishi. Sijawahi hata kumpigia simu.

SALEHJEMBE:Uliwahi kuitukana Yanga Kizaramo ukasema Mwali Kigego, kwa nini sasa Haji?
Manara: Shida yake hajui, halafu hataki kuuliza. Nilisema Kidile Mwali Kizika. Yaani mwali anayetoka, sasa ni tusi hilo?

SALEHJEMBE: Ulisema hukukopa, labda ilikuwaje?
Manara: Kweli sipendi kulizungumzia suala hilo, naweza kumuaibisha Jerry halafu ikaonekana kama namkashifu. Yeye ndiye aliomba fedha kulikuwa na msiba, sasa nitakuwa kama namsema marehemu, naona si uungwana. Kidogo nataka nitofautiane naye.


SALEHJEMBE:Utofautiane naye kwa maana ya mwonekano au nini, sijakuelewa.
Manara: Yeye anasema tu, hajui ukubwa wa Yanga. Mimi nautambua ukubwa wa Simba na heshima yake. Tunasikilizwa na kusomwa na watu wa aina zote. Sasa lazima kuonyesha heshima yako na wewe ni nani, si kwa kuwa msemaji basi kila kitu unasema.

SALEHJEMBE: Hadi mnachanganya, hivi kweli hamuelewani au mnatafuta kiki?
Manara: Ndiyo maana mambo mengine sitaki kujibu, yeye anataka kunitumia kupata kiki.


Siwezi kuruhusu hilo. Bora akiwa na hoja, basi aweke mezani tujadili hilo, si maneno ambayo hayaendani na watu au viongozi wa klabu kubwa kama Simba au Yanga. Mimi nimeamua kuchagua busara na aina ya mtu wa namna hii.
Si yule anayetaka kuzungumza kila jambo bila kulitafakari. Sitaki kuonekana nashindana, nafanya kazi ya Simba kwa maslahi ya klabu lakini kwa weledi.

SOURCE: CHAMPIONI0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV