Kocha Mkuu wa Yanga na vijana wake kwa siku mbili wamekuwa wakiangalia video mbalimbali za mechi za APR.
Mholanzi, Hans van Der Pluijm ataiongoza Yanga Jumamosi mjini Kigali kuivaa APR ya Rwanda katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hii ni baada ya kuwaondoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwenye michuano hiyo kwa mabao 3-0.
Pluijm alisema ni kama tayari wamewamaliza APR kabla ya mechi hiyo, baada ya kuzinasa video za wapinzani wao hao.
Pluijm alisema, video hizo za wapinzani wao, wamepanga kuzitazama benchi lote la ufundi pamoja na wachezaji wake kwa muda wa siku mbili mfululizo.
Aliongeza kuwa, video hizo alipanga kuanza kuzitazama kuanzia juzi Jumatatu jioni mara baada ya mazoezi na jana Jumanne wakiwa hotelini walipoweka kambi kwa kuwaangalia wachezaji wenye madhara kabla ya kukutana na wapinzani wao ili wajue jinsi ya kuwadhibiti.
“Ninaweza kusema kuwa, maandalizi tuliyoyafanya kwa ajili ya mechi dhidi ya APR yanakwenda vizuri kwa maana ya ndani ya uwanja, ikiwemo kuwapa mbinu mbalimbali za ndani ya uwanja kwa kukazania sana safu ya ushambuliaji ambayo inapoteza nafasi nyingi za kufunga.
“Kikubwa tunakwenda Rwanda kuvaana na APR kwa lengo moja la kurudi na ushindi na siyo kitu kingine, naomba niwatoe hofu mashabiki wa Yanga kwa hilo ni baada ya kunasa video za mechi za wapinzani wetu ambazo wamecheza.
“Video hizo tumeanza kuzitazama Jumatatu jioni baada ya mazoezi ya jioni, pia tutazitazama leo (Jumanne) baada ya mechi ya African Sports wakati tukiwa hotelini tukijiandaa na mchezo wa APR,” alisema Pluijm.
0 COMMENTS:
Post a Comment