April 4, 2016

CANNAVARO AKIWA NA KOCHA MSAIDIZI WA YANGA, JUMA MWAMBUSI.

Beki wa kati wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ametamka wazi kuwa hana wasiwasi na nafasi yake ndani ya Yanga kwani anaimani atarudi katika kikosi cha kwanza na kucheza kama zamani.

Cannavaro, ambaye baada ya kuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi mitatu, Alhamisi iliyopita alipata nafasi ya kucheza kwa dakika chache kwenye mchezo wa Kombe la FA, dhidi ya Ndanda na Yanga kushinda 2-1 amesema yupo tayari kwa mapambano tena.

“Tayari nimepona kabisa na nashukuru viongozi wangu wa Yanga kwa kunitafutia sehemu nzuri ya kunitibia majeraha yaliyokuwa yakinisumbua, nakishukuru pia Kituo cha Sunderland, kwani kwa muda wa wiki tatu kabla ya kujiunga na Yanga nilikuwa nafanya mazoezi pale ya kujiweka fiti.

“Nimerudi na sina wasiwasi na nafasi yangu kikosini kwani kwa nahodha yeyote duniani akirudi kutoka katika majeraha nafasi yake inakuwepo, naamini na mimi muda si mrefu nitaanza kuwa katika kikosi cha kwanza.

“Kikubwa nimefurahi nimepona muda muafaka ambao kila Mwanayanga anauhitaji mchango wangu na nasema kwamba nitawapa kile wanachokihitaji kwani nina hamu ya kucheza.

“Unajua miezi mitatu niliyokuwa nje imeniathiri kidogo, kwa sasa ninachofanya nimshawishi kocha ili aweze kunipa nafasi na niweze kucheza katika nafasi yangu niliyoiacha kwa muda mrefu,” alisema Cannavaro.


Ikumbukwe kuwa, kabla ya kuumia, alikuwa akicheza sambamba na Kelvin Yondani, lakini baada ya kuumia nafasi yake ikawa inashikiliwa na Mtogo, Vincent Bossou.

1 COMMENTS:

  1. Tuna hamu ya kumuona uwanjani tena na tena.

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV