April 22, 2016

BAADA ya Yanga kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika, timu hiyo imeangukia katika Kombe la Shirikisho Afrika ambapo huko imepangwa kucheza na Sagrada Esperança ya Angola.

Yanga imefikia hatua hiyo kwa kuwa kanuni za Ligi ya Mabingwa Afrika zinaeleza kuwa timu inayotolewa katika raundi ya pili, itashushwa mpaka kwenye Kombe la Shirikisho kucheza mechi mbili za mtoano na itakayosonga mbele itaingia robo fainali (hatua ya makundi).



Droo hiyo ilipangwa jana mchana ambapo pia kuna jumla ya timu nane kutoka Ligi ya Mabingwa na nane kutoka Kombe la Shirikisho. Yanga inatakiwa kuwa makini na mshambuliaji Arsénio Sebastião Cabúngula maarufu kwa jina la Love anayeichezea Sagrada Esperança.

Love licha ya kuwa na umri mkubwa wa miaka 37 lakini ndiye straika hatari ambaye anaongoza kwa mabao kikosini kwake na hata katika Kombe la Shirikisho yeye ndiye anayeongoza kwa mabao akiwa na mabao matano.



Rekodi zake msimu huu
Katika mechi ya kwanza ya hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho ya Sagrada Esperança dhidi ya Ajax Cape Town, timu yake ilifungwa mabao 2-1, hakufunga lakini katika mchezo wa pili wakiwa ugenini alifunga mabao mawili na kuiwezesha timu yake kusonga mbele.

Hatua iliyofuatia, raundi ya kwanza, Love akafunga bao moja na kuipa ushindi timu yake dhidi ya Liga Desportiva de Maputo ya Msumbiji, katika mchezo wa pili ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, akafunga tena bao moja.


Katika raundi ya pili, Sagrada Esperança ilianza kwa kushinda mabao 2-1 dhidi ya Vita Club Mokanda ya Congo Brazzaville ambapo Love alifunga bao moja.

Katika mchezo wa marudio timu yake ilishinda mabao 2-0 na hivyo kusonga mbele ndipo inakutana na Yanga.


Love ametoka wapi?
Huyu ni mzaliwa wa Luanda nchini Angola ambapo urefu wake ni futi 5 na nchi 11, kabla ya hapo aliwahi kukipiga ASA kuanzia mwaka 2000, baada ya hapo alipita katika timu kadhaa zikiwemo Primeiro de Agosto, Petro Luanda, Kabuscorp kisha akatua Recreativo da Caála mwaka 2014.
        
Katika timu ya taifa ya Angola alianza kuitumikia mwaka 2001 ambapo tangu hapo amecheza mechi 48 na kufunga mabao saba.

Amewahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Angola mara mbili mwaka 2004 na 2005, pia ameshatwaa mataji ya ligi kuu ya nchi hiyo maarufu kwa jina la Girabola mara tatu akiwa na kikosi cha ASA.

Mwaka 2006 alikuwemo katika kikosi cha taifa lake kilichoshiriki michuano ya fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Ujerumani.

Ratiba ya Kombe la Shirikisho kwa hatua ya mtoano inaonyesha kuwa mechi za kwanza zinatarajia kuchezwa kati ya Mei 6-8, mwaka huu, Yanga ikianzia nyumbani kisha marudiano ni kati ya Mei 17-18, 2016.

RATIBA YA MTOANO KOMBE LA SHIRIKISHO:
MO Béjaïa (Algeria)            Vs   Espérance   (Tunisia)

Stade Malien (Mali)           Vs    FUS Rabat (Morocco)
Étoile du Sahel (Tunisia)   Vs    CF Mounana (Gabon)
TP Mazembe (DR Congo)  Vs    Stade Gabèsien (Tunisia)
Al-Ahli Tripoli (Libya)        Vs     Misr El-Makasa   (Misri)
Al-Merrikh (Sudan)            Vs    K.Marrakech (Morocco)
Yanga (Tanzania)                Vs   Sagrada (Angola)
Mamelodi (Sauz)                 Vs  Medeama    (Ghana)

SOURCE: CHAMPIONI




1 COMMENTS:

  1. Hizi tabia za kutishana ndo huwa zinafanya wachezaji wetu wanacheza kwa hofu!!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic