April 2, 2016



Na Saleh Ally
MWENDO wa Simba kwenye Ligi Kuu Bara unaonekana kuwa bora zaidi ukilinganisha na matokeo yake ya karibuni. Iko kileleni ikiwa na pointi 57.

Yanga na Azam FC, zinaifuatia zikiwa na idadi ya mechi 21 na kila moja imekusanya ponti 50. Timu zote mbili, zina mechi tatu mkononi na kama zikishinda zote zitakuwa na pointi 59, maana yake zitashuka.

Inaonekana ni presha kubwa sana kwa Yanga na Azam FC kwa kuwa pamoja na viporo, kwa haraka zilitakiwa kucheza hadi mechi sita mfululizo. Yaani tatu za viporo vya ligi kuu, moja ya Kombe la Shirikisho (Kombe la FA) na mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

BAYERN

Ukiangalia haraka, utagundua sasa presha kubwa iko kwa Yanga na Azam kuliko Simba ambayo imecheza mechi nyingi ikashinda na sasa inaongoza kwa tofauti ya pointi saba ambazo ni mtaji mkubwa na presha kwa wapinzani wake.

Awali ilionekana kama Simba inatangulia kazi bure, lakini ushindi wake mfululizo umekuwa tatizo na mifano ipo. Mwanzo Yanga na Azam zilifeli katika viporo vyake baada ya kufungwa na Coastal Union.

Inaonekana kuwa na pengo la pointi ni bora zaidi kuliko viporo. Pia kuwa na pengo la pointi kunaongeza presha kwa wengine.

PSG
Ufaransa:
Nchi nyingine ambako kuna pengo kubwa ni Ufaransa. PSG inaonekana tena haitakuwa na wa kuizuia kubeba ubingwa wa League 1. Tofauti ya pointi 22 na Monaco inayoshika nafasi ya pili.

PSG tayari wana pointi 77 wakati Monaco wakiwa na 55. Kila timu imecheza mechi 31, zimebaki saba tu. Maana yake PSG ni bingwa tayari, hata ikifungwa zote na Monaco ikishinda zote itafikisha pointi 76.

BARCELONA

Hispania:
Barcelona nayo imetengeneza pengo kubwa La Liga. Inaonekana angalau Atletico Madrid ndiyo wanaoifukuza lakini wanatofautiana nayo kwa pointi 11.

Pengo hilo linazidi kutengeneza presha kwa Atletico kwa kuwa imeanza kuamini ubingwa ni mali ya Barcelona yenye pointi 76 kileleni, Atletico ina 67. Nafasi ya pili pia ina presha maana Madrid ina pointi 66 na lolote linaweza kubadilika.

Timu hizo zinalingana michezo, kila moja imecheza 30, ndani ya michezo 8, kuipiku Barcelona pointi zote 11 au 10, hii ni ndoto.

LEICESTER

England:
Hii ndiyo ligi yenye presha kubwa duniani, ikiwezekana pia ni ngumu na haitabiriki, tayari aliye kileleni ametengeneza pengo la pointi tano.

Leicester City iko kileleni na pointi 66, inafuatiwa na Tottenham yenye 61 wakati aliye nafasi ya tatu Arsenal ana pointi 55 na mchezo mmoja mkononi.

Utaona kama ilivyo katika ligi ya Tanzania. Kiporo kinaweza kisiwe na faida kama mlaji hatakuwa makini.

Leicester inaendelea kufaidika na pointi mkononi na pengo ililotengeneza. Kama itashinda mechi tatu mfululizo, maana yake itakuwa na pointi 75, huenda ikawa na uhakika wa kuwa bingwa kwa sare pekee katika mechi zake zilizobaki.

Hali kadhalika, Ujerumani na Ureno pia kuna pengo la pointi tano. Bundesliga, Bayern Munich inaongoza ikiwa na pointi 69 ikifuatiwa na Borussia Dortmund yenye 64 na mwenendo wa Bayern pia inaonyesha wazi, pengo litatumika vizuri na itabeba ubingwa. Mechi 9 zimebaki, lakini angalau ishinde nne zijazo, itakuwa na uhakika.

JUVE

Italia:
Kwenye Serie A, bado hakijaeleweka vizuri sana. Timu zote kila moja imecheza mechi 30. Juventus inaongoza kwa tofauti ya pointi 3 tu dhidi ya Napoli, zimesalia mechi 8.

Pengo hilo bado halina uhakika kama unavyoona kwenye Ligi Kuu ya Uholanzi ambako Ajax inapishana kwa pointi 2 tu na wapinzani wao wakubwa PSV.

Katika ligi hizi inaonyesha pengo linapokuwa dogo, presha inakuwa kubwa zaidi kwa aliye juu kama unavyoona kwa Juventus na Ajax.

Presha inapokuwa kubwa sana, unaona anayeteseka zaidi ni aliye katika nafasi ya pili au tatu kama unavyoona Tanzania, England na Hispania. Hii ndiyo raha ya pengo ambayo inapatikana kwa timu moja kufanya vizuri kwa kushinda mfululizo.


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic