AVEVA.. |
Na Saleh Ally
HIVI karibuni Simba imebadili mwendo kabisa kiutendaji na hasa uwanjani na kikosi hicho kimebadilisha mambo kutoka timu iliyokuwa haina nafasi ya kuwania ubingwa, sasa ni kati ya klabu tatu zinazopewa nafasi kubwa.
Simba iko kileleni ikiwa na pointi 57, inafuatiwa na Yanga na Azam FC, kila moja ikiwa na pointi 50. Timu hizi mbili zina mechi tatu mkononi, kwani Simba imecheza 24 na zenyewe kila moja mechi 21.
Pamoja na kasi nzuri ya Simba lakini kumekuwa na matatizo kadhaa kama yale ya utovu wa nidhamu wa wachezaji wake makinda kama Hassan Isihaka na Abdi Banda dhidi ya Kocha Jackson Mayanja. Pia kuna suala la fedha za Emmanuel Okwi ambazo Simba inaelezwa kulipwa na Etoile du Sahel na mengine mengi.
Kwa kuwa uongozi Simba umekuwa kimya sana, Lakini leo nu mahojiano kati ya SALEHJEMBE na Rais wa Simba, Evans Elieza Aveva, lengo ni kujua kuhusiana na hilo, pia mambo mengine ya maendeleo ya klabu hiyo.
SALEHJEMBE:Kuna mabadiliko makubwa hasa kasi na mwenendo wa ukusanyaji wa pointi katika kikosi chako, nini hasa unaona mlikuwa mnakosea awali?
Aveva: Sidhani kama tulikosea sana, lakini mwamko upya wa viongozi, benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki limesaidia mabadiliko hayo unayoyaona sasa.
SALEHJEMBE:Unaweza kufafanua mwamko huo?
Aveva: Viongozi wamekuwa wakipambana sana, ingawa ni tokea mwanzo lakini uamuzi wao wa kubadili benchi la ufundi umechangia mabadiliko hayo, hata Kocha Mayanja baada ya kupewa nafasi hajatuangusha.
SALEHJEMBE: Mashabiki wamechangia mwamko, hujafafanua?
Aveva: Ndiyo, maana wanakwenda uwanjani kwa wingi. Najua, walikuwa wakikata tamaa baada ya kuona timu haifanyi vizuri lakini sasa wanakwenda uwanjani na kuiunga mkono kwa nguvu sana timu yao. Kwetu ni jambo ambalo tunalihitaji maana hata kauli mbiu ya Simba unaijua (Simba Nguvu Moja).
SALEHJEMBE: Je, tayari uongozi umejua alichokuwa akikosea Dylan Kerr hasa baada ya kuja kwa Mayanja?
Aveva: Nafikiri yapo mengi, lakini haya machache yako wazi kabisa na yamechangia mabadiliko. Moja ni suala la nidhamu, hili ni muhimu sana. Angalia nguvu, stamina na kasi ya Simba. Wakati ule dakika ya 70, tunaanza kutafutana, sasa unaona timu inacheza.
SALEHJEMBE: Vipi wachezaji wenu wanaonekana kutokuwa na malezi bora kinidhamu, mnapata muda wa kuzungumza nao kuhusu hili?
Aveva: Kweli tunazungumza nao sana kuhusiana na hili, hatupendi hili litokee. Huenda umri wao mdogo pia unachangia. Ndiyo ni nadra kusikia wachezaji kama Mbuyu Twite au Kelvin Yondani wakifanya makosa hayo. Bado tunaendelea kuzungumza nao.
SALEHJEMBE: Suala la Banda hadi sasa halijawekwa hadharani, nafikiri suala la nidhamu linatakiwa kuchukuliwa hatua mara moja, mfano mzuri Sunderland na Emmanuel Eboue, Fifa wamemuadhibu, wao wakafanya hivyo baada ya saa nne tu?
Aveva: Kweli, lakini litafanyiwa kazi. Adhabu tunazotoa si kuwakomoa au kuwaangamiza hawa vijana. Lengo ni kuwaweka sawa.
SALEHJEMBE: Timu yenu ya vijana sasa si bora kama ya misimu mitatu iliyopita?
Aveva: Kweli, lakini tunajitahidi pamoja na gharama kubwa za uendeshaji. Ingawa vizuri TFF ingeandaa ligi ya kueleweka ya vijana, si vema wawe wanacheza michuano isiyoendana na vijana. Au wabaki wakifanya mazoezi tu bila mashindano maalum ambayo yangekuwa na morali ya ukuzaji vijana.
SALEHJEMBE:Timu nyingi sasa zinalia kuhusiana na kushuka kwa mapato, Simba vipi?
Aveva: Tunaathirika kweli, lakini kikubwa si kulalamika na badala yake tunajipanga mfano utaona tunabuni mipango kama uuzwaji jezi na vifaa vingine na kadhalika.
SALEHJEMBE: Unafikiri itatosha kuwaweka vizuri kwa kipato na kipi hasa kimewashusha kimapato?
Aveva: Kuna mambo mengi sana, bado tunafanya uchunguzi na tathmini kitaalamu ili tuweze kutatua tatizo badala ya kulalamika.
SALEHJEMBE: Mmepokea fedha za Okwi, vipi mnakuwa wagumu kutangaza mnazo?
Aveva: Hili linanishangaza sana, hivi kila fedha iliyoingia Simba huwa tunatangaza. Vipi hiyo ya Okwi na nani ana uhakika tumepokea? Ingekuwa hivyo kwa nini tumueleze kila mtu. Ushauri wangu, waache tuendelee kupambana.
Tuna mengi ya kufanya sasa hasa suala la mechi za mwisho za ubingwa, tuna Kombe la FA, sasa tunasumbuka na maandalizi ya ujenzi wa uwanja. Jamani, tuacheni kidogo.
SALEHJEMBE: Uwanja nao umekuwa ni hadithi, nyie haiwachoshi kuihadithia kila mara kama wenzenu Yanga?
Aveva: Siwezi kuwasemea Yanga lakini mchakato wetu wa uwanja uko hatua za mwisho kabisa. Tayari tumekaa chini na mkandarasi, tunajua mahitaji hadi bei yake. Tuna maandalizi ya kujenga uwanja wa mazoezi na hosteli pia.
SALEHJEMBE: Lini rasmi mtaanza, ili isiwe hadithi ya Bunju milele?
Aveva: Tayari nimeunda kamati itakayokuwa inashughulikia hilo, hakika ina watu makini ambao ninaamini wakianza kazi, hutauliza tena swali hili. Ila watu watuamini, ujenzi unaanza hivi karibuni ingawa mvua imekuwa ikitukwamisha.
SALEHJEMBE: Mvua inawakwamisha vipi, mnataka kutumia maji ya mvua?
Aveva: (Kicheko), Hofu ya mvua ni kwa kuwa mkandarasi amesema pale lazima pachimbwe. Kama itakuwa kuna mvua za masika, kutakuwa na tatizo na tutaingia gharama kubwa zaidi.
SALEHJEMBE: Kwa ufupi, uwanja mnataka uwe tayari lini?
Aveva: Pre season ya msimu ujao, Simba itafanya mazoezi kwenye uwanja wake.
SALEHJEMBE: Vipi biashara ya jezi mliyoanzisha hasa yale maduka, inalipa?
Aveva: Kiasi chake, imekuwa ikipanda na kushuka kutokana na matokeo ya timu. Mashabiki wanataka kuona ladha ya mpira wa Simba na ushindi, hilo tunalijua na tunapambana. Nawashauri mashabiki wajitokeze zaidi.
SALEHJEMBE: Mimi sielewi kuhusu Mayanja, ni kocha mkuu au msaidizi?
Aveva: (tabasamu), Mayanja kwa sasa ndiye kocha mkuu lakini tutatafuta kocha msaidizi ili tumtangaze rasmi.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment