April 4, 2016

FARID...

Kiungo kinda wa Azam FC na Taifa Stars, Farid Mussa, ameingia mkataba wa awali na Kampuni ya Vifaa vya Michezo ya Puma yenye maskani yake nchini Ujerumani.

Puma ambayo mbali na kuzidhamini klabu mbalimbali kama Arsenal, pia inawadhamini wachezaji maarufu akiwemo Sergio Kun Aguero wa Manchester City, Olivier Giroud (Arsenal), na wengine wengi.


Farid alisema bado mkataba haujawa rasmi lakini tayari kampuni hiyo ishaanza kumpa vifaa hivyo vya michezo na atakuwa akivitumia huku akiandaliwa safari ya kutua nchini Hispania kwa ajili ya kufanya matangazo.

“Ni kweli nitakuwa nadhaminiwa na Puma, lakini mkataba huo bado haujawa rasmi, tayari wameshanitumia vifaa ambavyo nitakuwa navitumia kwa sasa ikiwemo viatu vya kuchezea, ‘track suit’ na vifaa vingine.

“Vifaa hivi wamenitumia hivi karibuni lakini nikiwa klabuni siwezi kuvaa track zao, bali nitakuwa navaa nguo za Azam lakini nikiwa nje ya hapo nitakuwa navaa. Pia hivi karibuni kuna safari wameniandalia natakiwa kwenda Hispania na huko ndipo nitamalizana nao kwa kila kitu na kujulikana mkataba huo ni wa muda gani.

“Katika vifaa walivyonitumia ni viatu pea nne ambavyo vinaweza kufikia kama shilingi milioni moja na nusu za Kibongo,” alisema Farid.

Kampuni hiyo iliyoanzishwa mwaka 1924 na Mjerumani, Rudolf Dassler, pia inawadhamini watu wengine maarufu akiwemo mdogo wa Kim Kardashian, Kylie Jenner, na mwanaridha kutoka Jamaica, Usain Bolt.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV