May 28, 2016


Kama kawaida yake! Ikiwa ni siku ya kwanza tangu kufunguliwa kwa tamasha pendwa la Majimaji Selebuka tayari vituko, mbwembwe kutoka kwa viongozi wa kiserikali vimeanza kujitokeza hii ni baada ya Diwani wa Kata ya Matalawe Manispaa ya Songea, Judith Mbogoro kuibuka kinara wa mbio za Km 5 kwa upande wa wanawake.

Tamasha hilo limekata utepe leo Mei 28 na litafika tamati Juni 4, mwaka huu na linaganyika kwenye Uwanja wa Makumbusho ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji mjini Songea, Ruvuma.


Judith alitumia muda wa dakika 27:28, akifuatiwa na Fatuma  Ching’ang’a aliyetumia dakika 28:46 huku Theresia Tembo akimaliza wa tatu akihitimisha kwa muda wa dakika 30:26.

Akizungumzia ushindi wake, Judith alisema siri ya ushindi kuwa ni mazoezi kila siku, kupumzika muda mrefu na mlo mzuri.


“Tofauti na Jumapili kila siku nafanya mazoezi nazunguka uwanja wa mara tano, sinywi pombe, nalala muda wa kutosha (masaa 8) na kula vizuri (diet) ndiyo maana nimeweza achilia mbali umri wangu kunitupa mkono (miaka 38),” alisema Judith.


Kwa upande wa wanaume, kinara alikuwa Hamad Rashid aliyetumia dakika 16:59, nafasi ya pili Ferdinand Haule aliyetumia dakika 18:22 wakati nafasi ya tatu ilichukuliwa na Nathan Mpangala aliyetumia dakika 29:19 ambaye mbali na ushiriki huo, pia ni balozi wa tamasha.

Katika mbio za Km 21, John Mahagula aliibuka kinara kwa kutumia muda wa saa 1:32: 14, Jackson Faustine nafasi ya pili saa 1:41:17 na nafasi ya tatu ilichukuliwa na  Abdallah Oscar aliyetumia muda wa saa 1: 50:48.Washindi wote wameondoka na vitita vya fedha taslim, medali na vyeti vilitolewa kwa washiriki wote.

Kesho Jumapili ni mashindano ya Ngoma za Asili, maonyesho ya ujasiriamali pamoja na utalii wa ndani katika vivutio vya mbuga za wanyama.0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV