May 18, 2016

KESSY
Baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili ya kuichezea Yanga, beki wa kulia Hassani Kessy ameonekana anataka namba kwenye kikosi cha kwanza cha Mholanzi, Hans van Der Pluijm baada ya kuanza kujifua milimani.

Beki huyo, alisaini mkataba huo wa kuichezea Yanga kwa dau la Sh milioni 40 kwani mkataba wake na Simba unamalizika mwishoni mwa mwezi huu.

Kessy anatarajiwa kukutana na ushindani wa namba kutoka kwa Juma Abdul ambaye ameonekana kuwa tishio kutokana na kiwango chake kuongezeka kwa kiasi kikubwa na kumuweka benchi mkongwe, Mbuyu Twite.

Kessy alisema yeye hajapumzika na anautumia muda huu aliokuwa nje ya timu kwa ajili ya kufanya mazoezi binafsi kwa kukimbia mbio fupi na ndefu kwenye milima ya Morogoro alipokwenda kuisalimia familia yake.

Kessy alisema, tofauti na kukimbia mbio hizo, pia anafanya mazoezi ya gym na kuchezea mpira kwenye Kituo cha soka cha Morogoro Youth kilichomlea yeye na akina Shomari Kapombe wa Azam FC na Salim Mbonde wa Mtibwa Sugar.

 “Mimi hivi sasa nipo nyumbani kwetu Morogoro nilipokuja kukaa na familia kwa muda baada ya kusimamishwa Simba, lakini nikiwa huku natumia muda huu kwa ajili ya kujiweka fiti zaidi mara nitakapojiunga rasmi na Yanga nitakuwa kwenye kiwango kikubwa.

“Hivyo nimetengeneza programu maalum ninayoifanya asubuhi ninafanya mazoezi ya kukimbia milimani na kwenda gym, pia jioni ninakwenda kufanya mazoezi kwenye akademi iliyonilea kisoka.

“Ninajua ninakwenda kwenye timu yenye changamoto kubwa ya ushindani wa namba, hivyo ni lazima niongeze muda wa kufanya mazoezi kwa nguvu zote kuhakikisha ninapata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza,” alisema Kessy.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV