May 18, 2016

KIIZA, SIKU ALIPOTUA SIMBA...
Taratiibu mambo yanaanza kutimia baada ya uongozi wa benchi la ufundi la Simba, "kumchinjia baharini" mshambuliaji wao Hamisi Kiiza raia wa Uganda kwa tuhuma za utukutu au utovu wa nidhamu.

Si Kiiza tu, Waganda wenzake pia Juuko Murshid na Brian Majwega pamoja na Mkenya Paul Kiongera na Mrundi Emery Nimubona waligomea safari ya kwenda Songea kucheza mchezo huo kwa shinikizo la kulipwa kwanza mshahara wao ambao zilikuwa zimepita siku tisa tu.

Mbali na kuukosa mchezo huo, pia waliukosa mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar wikiendi iliyopita ambao Simba ilishinda bao 1-0 ugenini lililofungwa na Abdi Banda.

Simba inatarajia kuanza mazoezi leo Jumatano kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini huku kesho Alhamisi ikitarajia kuingia kambini kujiandaa na mchezo wa kufunga pazia dhidi ya JKT Ruvu inayosaka ushindi wa lazima ili ibakie Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Mratibu wa Simba, Abbas Ally Suleiman ‘Gazza’ amesema hawako tayari kuwa na wachezaji hao kambini kwani hakuna taarifa zao rasmi za kutokuwa na timu wiki mbili sasa.

“Kama mratibu sina taarifa za kwanini hawapo kikosini, siwezi kupokea wachezaji ambao hawapo nasi wiki mbili sasa na sitarajii kumtafuta mtu yeyote kuingia kambini na hata kama wakija wenyewe bado hawawezi kupokelewa mpaka kuwe na taarifa kutoka uongozi wa juu. Huo ndiyo msimamo wa benchi la ufundi,” alisema kiungo huyo wa zamani wa Lipuli FC.

Kocha Jackson Mayanja kuelekea mchezo na Mtibwa alisisitiza kuwa, anaamini vijana waliocheza mechi na Majimaji wana uwezo wa kupambana kwenye mechi zilizobaki.


“Mimi sina taarifa zao kwanini hawapo kambini, akili yangu ni kuhakikisha vijana nilionao wanaweza kupambana na tukamaliza katika nafasi ya pili ambayo inatafutwa pia na Azam FC,” alinukuliwa Mayanja.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV