May 18, 2016

KAMUSOKO
Siku chache baada ya kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu Bara, kiungo wa Yanga Mzimbabwe, Thabani Kamusoko, amewataja watu waliochangia kuipa timu hiyo taji la ubingwa msimu huu.

Timu hiyo ilikabidhiwa rasmi kombe la ubingwa wikiendi iliyopita baada ya kucheza na Ndanda na kutoka sare ya mabao 2-2.

Mzimbabwe huyo, huo ndiyo ubingwa wake wa kwanza kuutwaa tangu ajiunge na timu hiyo kwenye msimu huu wa ligi kuu akitokea FC Platinum akiwa na mwenzake, Donald Ngoma.

Kamusoko alisema shukrani na pongezi kubwa ziende kwa benchi la ufundi la Yanga lililo chini ya Kocha Mkuu Mholanzi, Hans van Der Pluijm na msaidizi wake Juma Mwambusi ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa wao kupata ubingwa huo.

Kamusoko aliwataja mashabiki nao kwani ndiyo waliotoa mchango mkubwa kwa kuisapoti timu yao wanapojitokeza uwanjani kwa ajili ya kuwapa sapoti kwa kuanzia Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na mikoani.

 “Ligi ilikuwa ngumu sana, lakini nashukuru sana benchi la ufundi kwa ushirikiano waliokuwa wanatupa wachezaji kuhakikisha tunafanikisha malengo yetu, pia mashabiki ninaamini bila ya wao tusingetwaa ubingwa huu.


“Pia nawashukuru benchi la ufundi kwa kunipa muda wa kuonyesha uwezo wangu ndani ya uwanja ambao ninaamini umeonekana, asante sana Yanga,” alisema Kamusoko.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV