May 4, 2016Mashabiki wa Yanga wamemvaa mshambuliaji wa Azam FC, Didier Kavumbagu na kumuomba kurejea kuichezea timu hiyo, mwenyewe akawaambia: “Tulieni nakuja huko.”

Tukio hilo la aina yake lilitokea Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakati mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Azam na Simba. 

Picha nzima ilianza hivi, Kocha wa Azam, Stewart Hall alimnyanyua Kavumbagu na wenzake wakapashe misuli moto, ndipo mshambuliaji huyo akaenda kufanya hivyo upande walipo mashabiki wa Yanga.

KAVUMBAGU WAKATI AKIWA YANGA...
Kavumbagu akiwa na wenzake Said Morad, Abdallah Heri na Mudathiri Yahaya, mashabiki wa Yanga wakaanza kumtupia maneno wakimtaka arejee kwenye klabu yao kwenye msimu ujao kwani Azam hapati nafasi ya kucheza.

Wakati mashabiki hao wakimpigia kelele hizo, mwenyewe aliwatuliza na kuwaambia kwa ishara ya mikono kuwa tulieni ninakuja huko huku akiibusu ‘bips’ yake aliyovalia juu ya jezi yenye rangi ya kijani na kuzusha kelele nyingi jukwaani huko.

Mara baada ya mechi hiyo kumalizika, Kavumbagu alipofuatwa ili azuzungumzie kitendo hicho, kwanza alicheka na kusema kuwa: “Wale aisee ni mashabiki wangu niliokuwa nao tangu nikiwa naichezea Yanga.

“Wakati napasha misuli upande wa jukwaa lao, walikuwa wakinisemesha na kuniambia nirudi Yanga, hivyo nikawatuliza kwa kuwaambia wasubiri ipo siku nitarejea kuichezea timu yao,” alisema Kavumbagu.


Kavumbagu hivi sasa ni mchezaji huru kutokana na mkataba wake wa mwaka mmoja wa kuichezea timu hiyo kumalizika, hivyo anaruhusiwa kujiunga na timu yoyote.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV