May 4, 2016
Hali si shwari kwani Kocha wa Stand United, Patrick Liewig, amewa-timua kikosini nyota wake watatu, Abuu Ubwa, Haruna Chanongo na Rajab Zahir lakini uongozi umemkatalia uamuzi wake huo.

Ubwa na Zahir kwa nyakati tofauti wamewahi kuitumikia Yanga kama ilivyo kwa Chanongo aliyewahi kuichezea Simba, kwa muda mrefu watatu hao hawakuwa na uhusiano mzuri na Liewig.

Ubwa amesema, ishu nzima ilianza wakati yeye na Chanongo walipoenda TP Mazembe kufanya majaribio ambapo baada ya kurejea visa vikaanza kocha akidai wameshuka viwango.

“Hapa juzi baada ya mechi na Mwadui (FC) kocha aliandika barua kwa viongozi kuwa sisi tusimamishwe, naona kabisa anataka kutuharibia maisha yetu ya kisoka jambo ambalo sisi hatupo tayari kuona linatokea.

“Mwenyekiti kwa upande wake amekataa kuzisaini kutokana na kutambua mchango wetu, viongozi wanaona kama tukiondoka basi tuondoke salama na siyo kama anavyofanya kocha.

“Nimepanga msimu utakapomalizika siongezi mkataba, bora nikatafute maisha kwingine,” alisema Ubwa.  

Mmoja wa viongozi wa Stand ambaye hakutaka jina lake litajwe, amethibitisha kupokelewa kwa barua hiyo ya Liewig raia wa Ufaransa lakini ‘wamechomoa’ kuisaini.

Inaaminika kuwa Liewig aliamini wachezaji hao wanajiona baada ya kutoka kufanya majaribio, hivyo anawafanyia visa waondolewe ili dili la kwenda TP Mazembe lishindikane. 

Liewig pia alikuwa kwenye mgogoro mkubwa wa muda mrefu na straika wa kutumainiwa wa timu hiyo, Elias Maguri kiasi cha kumpiga benchi kwa madai kuwa hataki mchezaji ajione staa katika timu yake.

SOURCE: CHAMPIONI 0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV