May 30, 2016Kocha wa zamani wa Toto Africans ya Mwanza, Mjerumani, Martine Grelics, amesema kuwa yupo tayari kuchukua jukumu la kuinoa Simba kwa msimu ujao na ikafanya vizuri.
Mjerumani huyo ambaye aliondoka katikati ya msimu uliomalizika hivi karibuni, kwa sasa yupo nyumbani kwao akifanya kazi ya kuwanoa wachezaji mbalimbali kwenye kituo chake cha soka cha Alpenkick Fussballschule.

Simba ambayo mwanzoni mwa mwaka huu ilimtimua kocha wao, Muingereza, Dylan Kerr na mikoba yake kuchukuliwa na Mganda, Jackson Mayanja, kwa sasa ipo kwenye mchakato wa kumleta kocha mwingine atakayesaidiana na Mayanja.

Licha ya majina ya makocha wanaotakiwa na Simba bado hayajawekwa hadharani, lakini jina la Muingereza, Boby Williamson aliyewahi kuinoa timu ya taifa ya Uganda, limekuwa likitajwa mara kwa mara kuchukua mikoba hiyo.

Grelics akiwa kwao Ujerumani, amesema tangu alipoondoka amekuwa akiendelea kulifuatilia soka la Tanzania na baada ya kuona msimu wa ligi umemalizika, akaona ni bora kuanza kusaka timu ya kuifundisha hapa Bongo na kuona Simba inahitaji kocha, hivyo yupo tayari kuifundisha.

“Nipo kwenye mchakato wa kurudi tena Tanzania kufundisha soka kwani maisha niliyoishi awali nilipokuwa na Toto Africans, nilibaini kwamba Watanzania ni wakarimu sana.


“Kwa sasa naangalia ni jinsi gani naweza kutuma CV zangu kwenye Klabu ya Simba, endapo nitapata jukumu la kuinoa Simba, wala wasiwe na wasiwasi kwani kwa uwezo nilionao naamini nitaipa mafanikio makubwa Simba,” alisema Grelics.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV