May 30, 2016Straika wa Yanga, Mzimbabwe, Donald Ngoma, amesema wazi kuwa haifahamu sana TP Mazembe ya DR Congo lakini atakapokutana nayo atahakikisha anaifunga.

Hiyo imekuja baada ya Yanga kupangiwa TP Mazembe kama moja ya timu zilizopo kwenye kundi lao la Kombe la Shirikisho Afrika, timu nyingine ni Medeama ya Ghana na MO Bejaia ya Algeria.

Ngoma amefunguka kuwa kilichobaki sasa ni kupambana na siyo kuangalia wanawafahamu vipi wapinzani wao, hivyo hata kama hawajui, hiyo haiwezi kuzuia wao kupigania matokeo yaliyo bora kwao kwa ajili ya kuzidi kusonga mbele.

“Siwafahamu Mazembe kwa kiasi kikubwa lakini shida yetu ni kupata matokeo mazuri yenye faida kwetu, tutapambana na lengo letu ni ushindi tu, kuwafunga itakuwa matokeo mazuri zaidi kwetu, kwa hiyo kilichopo ni kutafuta ushindi tu,” alisema Ngoma aliyeifungia Yanga mabao 17 kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

Yanga inatarajia kuikaribisha Mazembe kati ya Juni 28 au 29 katika mchezo wa nyumbani kabla ya kurudiana huko DR Congo kati ya Agosti 23 au 24, mwaka huu. 


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV