May 3, 2016


Na Saleh Ally
Hauwezi tena kukataa katika mchezo wa soka nchini kuna vitendo vya rushwa ndiyo maana tendo hilo limekuwa gumzo mwishoni mwa ligi kuliko hata wingi wa pasi wa timu fulani.

Rushwa inazungumzwa hata kuliko ubora wa washambuliaji wa timu kadhaa au ubora wa timu fulani katika ulinzi.

Gumzo la rushwa, limechukua sehemu kubwa ya mazungumzo ya mechi za mwisho za Ligi Kuu Bara.

Viongozi wana hofu, wachezaji pia wana hofu. Mashabiki wa kila upande wameanza kuamini kuna mchezo mchafu kutoka upande mwingine.

Fulani “anacheza” mechi zetu ndiyo gumzo ambalo linasherehesha kwamba rushwa katika soka ipo.

Tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) iko kazini ikilifanyia kazi sakata la viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutuhumiwa kupatikana wakipanga matokeo ya daraja la kwanza.

Jiulize, kwa nini sasa rushwa ndiyo gumzo kuliko mpira wenyewe wa soka. Je, kweli bingwa anayepatikana huwa ni Bingwa wa Rushwa?

Kama ni hivyo imeanza lini, kama ni hivyo safari iliyopita au miaka minne au 10 iliyopita ilikuwa ni mara ya ngapi?

Tuamini wanaosema au kuamini rushwa ipo ni wale walioshindwa kupambana sasa wanatafuta sababu zisizokuwa na msingi?

Au tuchague kuwasikiliza na kuangalia kama kuna tatizo? Au pia tujiulize vipi wanajua kila kitu, kwani nao waliwahi kushiriki?

Kwa sasa, kinachoonekana lazima tukubali. Tuweke ushabiki kando, tuache maneno mengi na tukubali udhaifu kwamba rushwa katika soka ipo.

Rushwa imekuwa msingi wa mafanikio kwa wengine. Wako wanaingia katika uamuzi na ndoto yao ni kufikia kuchezesha ligi kuu ili wapate rushwa za kutoka katika timu mbalimbali.

Wako mawakala wa kufikisha rushwa kwa waamuzi, wako mawakala wa kufikisha rushwa kwa viongozi wa mashirikisho na vyama na viongozi wa klabu zote kubwa, ndoto na nyinginezo wanajua kuna rushwa ila wanajikausha tu.

Kweli suala la rushwa ni siri kubwa, wahusika wakikosolewa ni wakali kama hawapendi na wanajenga uadui na wakosoaji. 

Lakini ukweli ni huu, rushwa ipo na ifikie ambao mnashiriki muache. Wimbi la ushiriki wa rushwa ni kubwa, pana na mtandao ni mkubwa.

Wahusika mnajitambua lakini hii ni hali halisi. Kama rushwa ndiyo itakuwa msingi na ikafikia tunazungumza rushwa zaidi ya mpira wenyewe. Basi mjue tumekwisha na tutabaki hapa milele.0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV