May 6, 2016Watu wengi hawajui sababu hasa za Simba kushindwa kufanya vizuri msimu huu licha ya kujipanga kwa mapambano, lakini Kocha wa Simba, Mganda, Jackson Mayanja, ametaja sababu kubwa ya wao kuboronga kila siku zinavyozidi kuyoyoma kuelekea kumalizika kwa msimu.

Simba wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 58 nyuma ya vinara, Yanga wenye pointi 68, inaonekana kama hawana uwezo tena wa kutwaa taji la ligi kuu msimu huu.

Simba iliuanza vizuri msimu huu kwa kuvunja baadhi ya rekodi zilizokuwa zikiwasumbua kwa miaka mingi ikiwemo ile ya kuibuka na ushindi kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ikiwa chini ya Kocha Dylan Kerr.

Mayanja ambaye amechukua mikoba ya kuinoa Simba mara baada ya Kerr kutimuliwa Januari, mwaka huu, amesema ufinyu wa kikosi chake ndiyo sababu kubwa ya Simba kuboronga kwani wanashindwa kuendana na kasi ya ligi.

“Angalia kikosi cha Azam kisha angalia cha Yanga, utagundua kwamba vikosi vyao ni vipana sana na vina wachezaji ambao akikosekana huyu basi anayechukua nafasi yake anaonekana hana tofauti na yule wa kwanza, hiyo kwetu inatupa shida kidogo.

“Ufinyu wa kikosi changu tofauti na Yanga na Azam ndiyo sababu kubwa iliyotufelisha katika kuwania mataji msimu huu, kama ningekuwa na kikosi kipana kama vya timu hizo sidhani kama Simba ingekosa hata kombe moja,” alisema Mayanja.


Kikosi cha Simba msimu huu kimekumbwa na majeraha ya wachezaji wake wengi wa kikosi cha kwanza huku wengine wakisimamishwa kwa utovu wa nidhamu ambapo hali hiyo ndiyo Mayanja anaamini imewarudisha nyuma kwani hakukuwa na watu sahihi kama mbadala wao.

1 COMMENTS:

  1. Hakuna kocha hapo angalia miaka 4 aliyokuwa kagera kafanya kitu gani na hata miezi sita ya Coastal hadi kutimuliwa?Aveva anapenda vya kunyonga vya kuchinja haviwezi ndio maana kaleta mtoa ushauri katika timu badala ya kocha.Huyo Mayanja kila kukicha yeye na magazeti tuu sasa huo mpira anafundisha muda gani?Kutwa ooh Yanga jeuri,mara Azam wababe tena marefa hawafahi sasa tushike lipi na wakati wachezaji wake anawafukuza?
    Mayanja pamoja na huyo Manara wetu hakuna cha kujivunia pale!

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV