TAMBWE... |
Mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara Mrundi, Amissi Tambwe amewatoa hofu mashabiki wa Yanga, akiwaambia: “TP Mazembe kitu gani, lazima wakae.”
Kauli hiyo, ameitoa ikiwa siku chache tangu Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kufanya droo ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa Yanga kupangwa Kundi A na Timu za MO Bejaia (Algeria), Medeama (Ghana) na TP Mazembe huku Kundi B, likiwa na Kawkab (Morocco), Etoile du Sahel (Tunisia), FUS Rabat na Ahly Tripoli ya Libya.
Mrundi huyo, kwenye msimu huu wa Ligi Kuu Bara ameweka rekodi ya pili ya kuchukua ufungaji bora kwenye ligi akifunga mabao 21 huku akiwapita Hamis Kiiza mwenye mabao 19 na Donald Ngoma aliyefunga mabao 17.
Tambwe alisema soka la Afrika limebadilika kwa kiwango kikubwa, hivyo haoni sababu ya kuwahofia wapinzani wao Mazembe.
Tambwe alisema, katika kuthibitisha hilo, wamepanga kushtusha watu kwa kuwaondoa Mazembe na kutwaa ubingwa huo, mwaka huu na hilo linawezekana kutokana na ubora wa kikosi chao.
“Ni mbaya kuishi kwa mazoea kama ilivyokuwa kwa Mazembe ambao wanapewa nafasi kubwa ya kututoa kwenye hatua ya makundi Afrika kitu ambacho siyo sahihi.
“Nikuhakikishie tu, soka la Afrika limebadilika kwa kiwango kikubwa, hao Mazembe wanaopewa nafasi kubwa ya kututoa, niamini tunawatoa wao na kuchukua ubingwa huo na kama unabisha subiria uone.
“Hayo ndiyo malengo tuliyojiwekea na hilo linawezekana kutokana na ubora wa kikosi chetu kinachoundwa na wachezaji wengi wenye uzoefu wa michuano hiyo,” alisema Tambwe.
0 COMMENTS:
Post a Comment