Beki mpya wa Simba, Hassan Kessy, hataonekana nchini kwa muda wa siku 14 akitarajiwa kuonekana siku tatu kabla ya mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Anakwenda Ulaya na hiyo itakuwa safari yake ya kwanza akiwa na Yanga itakayokwenda kuweka kambi yake nchini Uturuki kujiandaa na mechi ya MO Bejaia ya Algeria na Mazembe.
Yanga inaondoka kesho Jumapili kwenda Uturuki na haitaonekana tena hadi Juni 28, mwaka huu itapovaana na wapinzani wao TP Mazembe.
Safari hiyo, itawajumuisha wachezaji wengine wapya Juma Mahadh, Vincent Andrew ‘Dante’ na Beno Kakolanya ambao hiyo itakuwa safari yao ya kwanza tangu watue kuichezea Yanga.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa Yanga, timu hiyo kabla ya kwenda Algeria kuvaana na MO Bejaia, kwanza itatua Uturuki kwa ajili ya kambi ya muda mfupi na baadaye kuondoka.
Chanzo hicho kilisema, Yanga mara baada ya mechi na MO Bejaia itakayopigwa wikiendi ijayo, watarejea tena Uturuki na kupiga kambi ya siku tisa kuanzia Juni 20 hadi 26 watakapofika jijini Dar es Salaam siku mbili kabla ya mechi na Mazembe.
“Timu inaondoka keshokutwa (kesho Jumapili), lakini haitaenda moja kwa moja Algeria badala yake tutaweka kambi ya siku chache nchini Uturuki na baadaye tutaelekea Algeria kwa ajili ya mechi na MO Bejaia.
“Mara baada ya mechi na MO Bejaia, timu itarejea tena Uturuki kwa ajili ya kambi ndefu kidogo ya siku kama tisa kuanzia Juni 20 hadi 26 na timu itarejea Dar siku mbili kabla ya mechi na Mazembe tutakayoicheza Juni 28,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, Yanga inaondoka bila ya nahodha wake Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Juma Abdul. Cannavaro anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa katika mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Sagrada Esperanca wakati Abdul ana maumivu ya enka.
0 COMMENTS:
Post a Comment