June 12, 2016
Na Saleh Ally
Nimeiona hii picha mtandaoni, kwanza hongera kubwa kwa mpigaji ingawa sijui ni nani.

Lakini nimeona niizungumzie kwa kuwa ni picha inayoonyesha hisia za dhati kutoka kwa walio katika picha hii. Soka ni mchezo wa wote na hasa watu masikini, hii picha inaanza kuonyesha hilo.

Ni picha inayozungumza mambo mengi sana ukitulia na kuiangalia. Nitaanza kukuelezea.

Moja:
Angalia watoto wanaocheza kwenye uwanja mbaya kabisa, uwanja ambao mtoto kutoka Ujerumani, England, Hispania au kwingineko Ulaya asingethubutu kukimbia hata kidogo, ni hatari lakini mapenzi ya soka yanawazidi nguvu watoto hawa ambao ninaamini ni kutoka Kenya, wanaendelea kuinjoy soka. SOKA INA NGUVU BANA.

Mbili:
Pamoja na kucheza katika sehemu hatarishi, watoto hawa hawana viatu vya soka maarufu kama njumu. Wamevaa Yeboyebo na ndiyo wanazozitumia kucheza. Hakika hiki ni kitu kinachoonyesha mapenzi yao ya juu kuhusu mchezo huu. Hakika, SOKA INA NGUVU BANA.

Tatu:
Watoto hawa hawana jezi, nguo zao za kawaida ambazo ndiyo wanategemea kuzivaa katika siku za kawaida, wanazitumia. Hawana sababu ya kuvua kwa kuwa wanaupenda mchezo wa soka. Hili nalo linaonyesha kweli mchezo wa soka unapendwa. SOKA INA NGUVU BANA.

Nne:
Kwa kuwa hawana jezi, watoto hao wameamua kufanya ubunifu wa juu kabisa. Wamechukua mifuko ya kuhifadhia bidhaa kutoka katika maduka maarufu ya Uchumi ambayo yalifilisika, wakaichana na kuivaa ili iwe kama jezi na wao wawe wadhamini wao. Hakika inaumiza moyo, lakini inavutia kuona watoto wa Kiafrika wenye moyo ya mapenzi ya juu na soka lakini wanaonyesha kutaka jezi au vifaa, kuvikosa kwao, ndiyo kunaamsha ubunifu huo. Nakukumbusha, SOKA INA NGUVU BANA.

Tano:
Angalia macho ya watoto hao, wanaonyesha wako busy na kitu bora, kitu cha uhakika. Wanataka kucheza washinde, wanataka kufanya vizuri na ushindani uko kwenye mioyo yao kwa dhati kabisa. Hakika, SOKA INA NGUVU BANA.

Mwenyezi Mungu awabariki, siku moja wafike mbali na kuwaonyesha vijana wengine masikini kwamba, hata kama ni fukara lakini hakuna anayeweza kukuzuia kutimiza ndoto zako kama ukiamua.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV