June 3, 2016

KOMBA
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) aliyewekwa kusimamia uchaguzi wa Yanga, Aloyce Komba, amejiuzulu nafasi hiyo kwa kile alichodai ni kutupiwa tuhuma nzito na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji.

Uchaguzi huo ambao TFF imepanga ufanyike Juni 25, mwaka huu, umekuwa na sintofahamu nyingi baada ya mapema wiki hii, Yanga nao kusema wao watafanya uchaguzi Juni 11, mwaka huu.

Komba alisema amefikia uamuzi huo, baada ya kuona kama akiendelea kuwepo katika nafasi hiyo, inaweza kutokea hali ya kuvuruga mambo ndani ya Yanga kitu ambacho yeye hapendi kitokee.

Alisema baada ya kuchukua uamuzi huo, hatojihusisha kwa namna yoyote ile na uchaguzi huo hata kutoa ushauri wala maoni. 

"Leo (jana) natangaza kujitoa kuwa Mwenyekiti wa Uchaguzi wa Yanga kama nilivyoteuliwa na TFF, nimefikia hatua hii kutokana na tuhuma nilizopewa na mmoja wa wagombea ambaye ni Yusuf Manji Juni 2, mwaka huu alipozungumza na waandishi wa habari.

“Manji alisema mimi nilipanga kumkata, hivyo kwa kushauriwa na watu wangu nikaona bora nikae pembeni.
“Kwa sasa naruhusu mamlaka husika zichukue nafasi yake kuchunguza kama kweli nimehusika na hizo hujuma, nimejitoa rasmi na majukumu yote namuachia makamu wangu, Domina Mideli," alisema Komba.

Wakati huohuo, TFF jana ilitoa taarifa inayosisitiza uchaguzi wa Yanga kufanyika Juni 25, mwaka huu licha ya Yanga nao kutangaza tarehe yao ambayo ni Juni 11, mwaka huu.
0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV