June 17, 2016




Na Saleh Ally
KIPINDI cha usajili kwa klabu, unaweza kukifananisha na mtu anayefanya ujenzi wa nyumba ambayo ataishi. Anatakiwa kuwa makini, mtulivu na anayefanya mambo yake kwa uhakika.

Kama nyumba ataishi baada ya kukamilika, hakika hatakiwi kuteleza hata kidogo kwa kuwa ikitokea hivyo ni kujiingiza matatizoni kwa muda mrefu sana. Ningeweza kulifananisha suala hili na mtu anayetafuta mke au mume, lakini tuliachie hapo.

Simba iko katika harakati za usajili, sasa ndiyo kipindi kizuri cha kufanya marekebisho kadhaa matika sehemu ambazo inaona zilikuwa na mapungufu katika misimu miwili iliyopita.

Chini ya Rais mpya, Evans Aveva, Simba imecheza misimu miwili na yote imeangukia katika nafasi ya tatu. Maana yake haijawa na nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa mara tatu chini ya uongozi huo.

Ukijumlisha na misimu mingine miwili chini ya uongozi wa mwenyekiti wa mwisho wa Simba, Ismail Aden Rage, Simba haijawa na mafanikio kwa misimu minne sasa. Hili si jambo dogo hata kidogo.

Wanachama na mashabiki wa Simba wanaumia kwa kuwa timu yao ni moja ya zile kubwa na maarufu kabisa barani Afrika. Hivyo wanahitaji kuona mabadiliko yanafanyika.

Waingereza wanasema “Changes is a process”. Mabadiliko ni hatua, kamwe Simba haiwezi kufanya usajili ambao inategemea uwe mabadiliko ndani ya siku mbili pekee, hilo haliwezekani hata kidogo.

Nimeona mashabiki au wanachama wa Simba wamekuwa na presha kubwa kuona wapinzani wao Yanga wakiendelea kusajili huku wao wakiwa kimya. Hii inaonekana kama kuwavunja nguvu hivi, jambo ambalo si kweli.

Simba haipaswi kufanya usajili wa mashindano, Simba haipaswi hata kidogo kufanya mambo ili ionekane, yaani ikimbie haraka ilimradi ijulikane imesajili. Lazima kuwe na mipango sahihi.

Mfano suala la ripoti ya mwalimu Jackson Mayanja ambaye alimaliza msimu akiwa na kikosi cha Simba. Inapaswa ifuatwe, lakini kuna wachezaji ambao wameondoka katikati ambao Simba itatakiwa kufanya utaratibu wa kuziba nafasi zao.

Yanga inaweza kuwa na haraka katika kipindi hiki kuhusiana na suala la usajili kwa kuwa ina majukumu ya michuano migumu ya Kombe la Shirikisho hatua ya robo fainali.

Sasa Simba wanataka kufanya usajili wa haraka, wanakimbilia wapi? Wanaweza vipi kufanya usajili ambao hauwezi kuwa na faida kwao halafu uwe tatizo kesho? Si sahihi Simba kufanya usajili wa kuwaridhisha mashabiki.

Vizuri mashabiki wakafurahishwa na matokeo hapo baadaye badala ya kufurahishwa na usajili kipindi hiki. Hivyo suala la usajili linapaswa kuwa la kitaalamu zaidi kuliko kuwa la kishabiki na kuwafurahisha mashabiki kwa kipindi cha sasa.

Nani amesema Yanga inaweza kusajili wachezaji wote wa Afrika au Tanzania na Simba ikakosa kabisa ikihitaji? Ninaamini kwa timu hizo zilivyo, hata mipango zinakwenda tofauti, moja inataka hivi na nyingine vile kulingana na upungu wa vikosi kutoka kila upande.

Kwa upande wa mashabiki nao wanapswa kuwa waungwana na kuheshimu kazi inayofanywa na kamati za usajili na ufundi na si kila mmoja kutaka kuonyesha anajua au kutaka kujifurahisha kwa kuona wachezaji wanasajili mfululizo.

Kama kamati hizo za Simba zitatulia na kufanya mambo yake kwa uhakika kipindi hiki, basi zitakuwa na nafasi ya kutengeneza timu bora kwa ajili ya msimu ujao.
Lakini kama kamati hizo, zitafanya usajili wa sifa, kutaka kuwafurahisha mashabiki na wachama kwa kipindi hiki kifupi, kwa mara nyingine Simba itaenda mwendo wa kusuasua msimu mwingine ambao tutahesabu wa tano, jambo ambalo halitakuwa zuri kwa mashabiki, wanachama na viongozi wenyewe.

SOURCE: CHAMPIONI



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic