June 1, 2016


Baraza la Michezo la Taifa (BMT), limemtaja mtu kutoka ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuhusika kwa namna moja ama nyingine juu ya kutaka uchaguzi wa Yanga usifanyike kama ilivyopangwa.

BMT iliiagiza Yanga kufanya uchaguzi wake kabla ya Juni 30, mwaka huu ambapo mchakato wake kwa sasa umeonekana kusuasua baada ya zoezi la uchukuaji fomu za kugombea nafasi mbalimbali kuonekana kuna gumu.

Kutokana na zoezi la uchukuaji na urudishwaji wa fomu kuonekana kusuasua, BMT imeamua kulisogeza mbele kutoka jana Jumanne ambayo ilitakiwa kuwa siku ya mwisho na sasa itakuwa ni Jumapili ya Juni 5, mwaka huu.

Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Mohammed Kiganja, amesema: “Tumelazimika kusogeza mbele zoezi la uchukuaji fomu kutokana na mambo yanayotendeka katika mchakato huu wa uchaguzi ambayo hayakubaliki.

“Tumebaini kwamba kuna mtu au watu wanataka uchaguzi usifanyike na hao watu wapo ndani ya TFF, sasa tunatoa angalizo kwa yeyote yule atakayeendelea kufanya hivyo hatutasita kumchukulia hatua na pia tunaiomba TFF imuonye mtu huyo kuacha kufanya hivyo mara moja.

“Mtu huyo tunamjua, kwa leo hatutapenda kumuweka hadharani lakini ifahamike tu ndiye anayehusika kuweka fomu za uchaguzi kwenye mtandao.”

Naye Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas amesema: “TFF ni taasisi kubwa na wanafanya kazi kwa kusaidiana, hivyo kama mtu huyo anayefanya mchezo huo wa kuchelewesha uchaguzi wa Yanga anajulikana basi BMT haina haja ya kumficha.”

Mpaka jana Jumanne mchana, watu watatu waliripotiwa kuchukua fomu ambao ni Aaron Nyanda, Edger Chigula na Paschal Laizer.

Wakati huohuo, serikali imemsimamisha Emmanuel Mlundwa pamoja na Chama cha Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST) kujishughulisha, kusimamia na kuratibu ngumi za kulipwa ndani na nje ya nchi ndani ya miaka minne kuanzia jana Jumanne mpaka Mei 31, 2020.


Hatua hiyo imechukuliwa baada ya PST hivi karibuni kuratibu pambano la ngumi za kulipwa hapa nchini kati ya Mtanzania, Thomas Mashali dhidi ya Muiran, Sadjad Meherab. Katika pambano hilo, Mlundwa ambaye akiwa kama Rais wa PST, aliruhusu vijana chini ya umri wa miaka 10 kupanda ulingoni huku akifahamu kwamba anavunja sheria za utumikishaji watoto huku pia wakimtumia Joyce Francis mwenye umri wa miaka nane ambaye alitumika kama mnadi mizunguko (Card Girl).

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV