June 25, 2016



Na Saleh Ally
HIVI karibuni kulizuka mjadala mkubwa kuhusiana na safu ya ulinzi ya timu ya taifa, Taifa Stars. Kwamba inatakiwa kupatiwa mabeki wapya kwa kuwa waliopo ni ‘wazee’.

Walengwa wa suala la uzee walikuwa ni Nadir Haroub Ali maarufu kama Cannavaro na Kelvin Patrick Yondani ambaye kwa wachezaji wenzake maarufu kama Cotton.

Waliokuwa wakiamini wachezaji hao ni wazee, hakuna aliyekuwa na nguvu ya kumtangaza mbadala wa mabeki hao, kwani kila waliotajwa walielezwa kuwa ni wale wanaoweza kuimarishwa.

Pamoja na kuonekana ni ‘wazee’, waliokuwa wanawataja walionekana hawana viwango vya hao wawili. Hii ilikuwa ni sehemu ya uthibitisho kwamba ni mabeki bora kabisa ambao Tanzania imewahi kupata.

Yondani ambaye amekulia kisoka katika Jiji la Mwanza, ni kati ya mabeki bora kabisa ambao Tanzania imewahi kupata ndani ya kipindi cha miaka 10.



Wanaosema ni wazee, huenda ni tabia ya Watanzania kuendelea kuwazeesha wachezaji wao bila kufanya tathimini za kutosha au wakati mwingine ni hisia za chuki ambazo hujenga hisia za uropokaji, ili mradi mtu amesema tu.

Kama Yondani ana miaka 32, vipi unaweza ukamuita mzee ukitaka astaafu au aonekane hafai? Wakati leo Simon Masaba mwenye umri wa zaidi ya miaka 35 anaendelea kucheza? Angalia Andy Mwesigwa wa Uganda mwenye umri zaidi ya miaka 34, bado anaendelea kucheza! Kweli umri umemtupa mkono kwa maana ya soka, lakini ni beki wa aina yake ambaye unaweza sasa kujadili zaidi kiwango chake kuliko umri.



Yondani ni beki aliyechukua ubingwa wa Tanzania Bara mara nyingi zaidi katika kipindi cha misimu saba. Hii inamfanya kuwa mchezaji aliyebeba ubingwa mara nyingi zaidi katika kipindi hicho.

Yondani ambaye alikuwa katika kikosi cha Simba kilichobeba ubingwa wa Tanzania Bara msimu wa 2009-10, amechukua ubingwa mara tano akiwa na Simba na Yanga katika kipindi cha misimu saba.

Msimu mmoja wa Simba ambao ni 2010-11, Yanga walibeba ubingwa, akaukosa na akiwa Yanga msimu wa 2013-14, Azam FC wakauchukua ubingwa nao akaukosa. Kwa misimu mingine yote mitano, miwili akiwa Simba na mitatu akiwa Yanga ameiwezesha kuwa bingwa.

Katika kipindi chote akiwa Simba na kuchukua ubingwa mara mbili, akiukosa mara moja, Yondani alikuwa akicheza katika kikosi cha kwanza. Baada ya kutua Yanga 2012, hadi leo ameendelea kucheza katika kikosi cha kwanza.

Hakuna anayekumbuka ubora wa juu kabisa wa Yondani, mchezaji ambaye ameendelea kuwa tegemeo katika kikosi cha Simba na Yanga kwa misimu saba tofauti na hakuna mwenye uwezo wa kusema ameshuka kiwango na hapaswi kucheza.

Akiwa Simba, rundo la mabeki wa kigeni walisajiliwa, lakini mwisho Yondani akaonekana ndiye bora na tegemeo. Hali kadhalika akiwa Yanga, hali kama hiyo imetokea kwa wachezaji mbalimbali walionekana wana uwezo mkubwa katika nafasi ya ulinzi na huenda iliaminika ni mwisho wa Yondani. Mwisho ikaonekana bila ya msaada wake, hakuna anayeweza kucheza kwa uhakika zaidi.


Unaujua ubora wa Cannavaro lakini anaweza kuwa bora zaidi kama atacheza pamoja na Yondani ambaye wachezaji wenzake walimpachika jina la Cotton wakimaanisha pamba kwa kuwa ni beki mwenye uwezo mkubwa wa kunyumbulika.

Yondani ni kati ya mabeki wa kati wenye kasi kubwa zaidi, lakini ni mwenye mwili laini unaoweza kubadilika au kugeuka kulingana na mazingira. Unaweza usijue kama hutamfuatilia kwa karibu kuwa ni mmoja wa walinzi wasiokuwa na makosa mengi.

Mara chache kusikia amefanya makosa kwa kuwa zaidi anaangalia kanuni za uchezaji wa beki. Anaweza akakosea siku yoyote lakini kiwango chake cha makosa kitaendelea kubaki chini kwa kuwa amecheza kwa miaka mingi bila ya kuingia kwenye kundi la mabeki ‘wanaochomesha’.

Uwezo wa Yondani unauona katika kipindi wengi wanamuona ni mzee, katika msimu mmoja anaisaidia Yanga kucheza Kombe la Shirikisho hatua ya robo fainali. Katika msimu huohuo, Yanga inabeba ubingwa wa Tanzania, Kombe la Shirikisho nchini na ilianza kwa kuchukua Ngao ya Jamii.

Usisahau, katika misimu yote saba, timu alizochezea zilikuwa bingwa au nafasi ya pili tu. Simba ilianza kushika nafasi ya tatu wakati akiwa nje ya kikosi hicho. Yondani huyo karibu katika kila msimu wa Simba na hata Yanga amekuwa ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi.

Kucheza mechi nyingi zaidi maana yake uko fiti zaidi, si majeruhi au mgonjwa na kwa uwezo ulionao kocha anakuamini. Hii inamfanya Yondani kuwa mmoja wa wachezaji bora kabisa katika kipindi cha miaka 10 ya Ligi Kuu Bara.

Nje ya uwanja, huenda hii ni hadithi nyingine bora kwa kuwa si rahisi kusikia ameonekana sehemu fulani. Hata katika Michuano ya Ndondo au ile ya mtaani pia ni nadra sana, si maarufu kama wale wengine ambao wakikosekana watu wanajiuliza.

Yondani amewajengea nyumba wazazi wake katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam. Hii inaonyesha ni mchezaji anayejitambua, asiyependa makuu na inawezekana ni nadra kumuona mtaani zaidi ya mazoezini na kwenye mechi.

Si mtu wa maneno, zaidi anafanya vitendo uwanjani. Ni mchezaji aliyekifanya kiwango chake kuwa bora kwa misimu lundo, mchezaji ambaye si rahisi kuingia kwenye skendo za mapenzi na nyota fulani, asiyekuwa katika vurugu na klabu yake akidai mshahara na mengi yanayoonyesha ni kweli anajitambua na anajua anataka nini katika soka.

Yondani hajawahi kusema anataka kwenda Ulaya, huenda hajawahi kuwa na ndoto hiyo, lakini ameendelea kuifanya kazi yake kwa ubora wa juu kabisa na kuna kila sababu ya kusema anastahili kuwa mfano kwa vijana wengi wanaokua kwamba mafanikio ya maisha bado yanaweza kupatikana hapa nyumbani.

Lakini mchezaji lazima alenge katika utendaji sahihi ambao utamsaidia kuwa bora kwa kiwango kinachotakiwa na siku akiamua kustaafu, watakaotaka kuvaa viatu vyake, wajipange kweli.

MISIMU:
2009/10: Simba
2010/11: Yanga
2011/12: Simba
2012/13: Yanga
2013/14: Azam FC
2014/2015: Yanga
2015/2016: Yanga

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic