July 20, 2016



Na Saleh Ally
WAKATI wa utoaji tuzo za wanasoka bora wa msimu wa 2015-16 zilizofanyika Jumapili, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, alizungumza mambo mengi sana, huenda ilikuwa ni sehemu ya kutoa machungu aliyonayo.

Lakini moja ya sehemu ambazo niliona zinamshinda kuzifanyia kazi kwa maana huenda alitamani angeweza kuwanyamazisha na waandishi wa habari, ni pale alipoanza kulaumu mambo kadhaa yanayoripotiwa na vyombo vya habari.

Malinzi alilalama kuhusiana na suala la vyombo vya habari kushambulia suala la ratiba kuwa na viraka kibao huku akisisitiza kwa kutoa mfano wa Uingereza kwamba wenyewe jiografia yao inawaruhusu kwa kuwa timu inaweza kusafiri sehemu moja, kwenda nyingine kwa saa tatu tu na hapa Tanzania haiwezekani.

Alikwenda mbali zaidi na kutoa mfano, kwamba ilimradi kila mmoja anaweza kumiliki chombo cha habari, basi anajiandikia tu.

Acha hivyo, alikwenda mbali zaidi na kusema yeye sasa amekuwa ni sawa na dodoki. Naamini kila mtu analijua dodoki, hili hutumika kutoa uchafu kwenye mwili wa binadamu au vinginevyo, hasa wakati wa kuoga.


Lakini inawezekana akiwa na maana ya kila mmoja anamshambulia yeye, jambo analoona si sawa.

Nafikiri Malinzi anataka kugeuka mfalme asiyetaka kuguswa, hataki kukosolewa na angerufahi sana kusifiwa huku akijua anachokifanya hakistahili sifa. Anataka kupata alama 100 kwa alichokifanya wakati kinastahili alama 10 au chini ya hapo.

TFF chini yake, inakwenda kwa kiwango cha chini zaidi hata kama utafananisha na ile iliyopita chini ya Leodegar Tenga. Yeye Malinzi analijua hilo, lakini anaonekana kutofurahishwa, ndiyo maana katika hafla ya utoaji tuzo, badala ya kuzungumzia njia na mafanikio ya ligi, huenda aliona aitumie kujisafisha na kutoa mfano kama ule wa Uingereza ambao unazidisha kumfanya awe dodoki zaidi, nitaeleza kwa nini.

Ambacho ninapinga au wanachopinga wanahabari na wapenda soka wengine, ni ratiba kuwa na viraka ambavyo havina sababu za msingi hata kidogo na kama vikitokea viwili vitatu kutokana na mambo yanayoeleweka, hakuna atakayelaumu.

Lakini viraka kwa kuwa Azam FC inatakiwa kwenda kushiriki michuano ya kirafiki kule Zambia. Vipi usigeuzwe dodoki?

Kuwa na ratiba ambayo haijui ndani yake kutakuwa na michuano ya Caf ambayo inakuwa inajulikana! Vipi usionekane dodoki?

Lakini jiulize, kama Uingereza wanaweza kupanga ratiba yao wakijua usafiri utakuwa ni saa 3, vipi Tanzania tunashindwa kupanga yetu tukijua usafiri utakuwa saa 12? Tofauti ya hapa nini? Waingereza wamesoma jiografia yao, sisi tunashindwaje kusoma yetu? Sasa hapa utaepuka vipi kuwa dodoki?

Ukiangalia alichokuwa akijaribu kujitetea Malinzi mbele ya Mgeni Rasmi, Mwigulu Nchemba, hakina maana hata kidogo. Nafikiri kile alichomalizia na kusema watafanya juu chini, kuhakikisha ligi inachezwa kwa ratiba yenye uhakika, ndiyo jambo la msingi sana na itaweza kusaidia yeye kuondoka kwenye huo udodoki alioutangaza.

TFF ilionyesha njia na kujitahidi sana kwenye soka la vijana. Nimesikia, nimeona wadau wengi tu wakisifia, hapa utaona hakukuwa tena na nafasi ya kiongozi yoyote wa TFF kuwa dodoki.

Waendeleze mambo mengi kama wanavyojitahidi kwa vijana, lazima watasifiwa na watu watakuwa tayari kusaidiana nao kwa kuwa watakuwa wakifanya kwa ajili ya kulisaidia taifa.


Kama TFF itaendelea kufanya mambo yake kwa maslahi ya wachache, mfano viongozi wake, au watu wake wa karibu, hakika itafeli na hakuna atakayeacha kusema na kulalamika, kufanywa dodoki hakuwezi kuwazuia au kuwafumba watu midomo.

Malinzi akumbuke wanaweza kupatikana wachache watakaokuwa tayari kumtetea kwa kuwa wanafaidika. Lakini hawawezi kushinda nguvu ya kweli ya wanaosema ukweli kwa kuwa wanayaona madudu ambayo hata mtoto wa darasa la tano anaweza kugundua ni madudu na TFF ya sasa, inaendelea kufeli kwa asilimia kubwa kuliko inavyofanya vizuri.

Chondechonde Malinzi, TFF ni ya Watanzania, hakuna anayeweza kukupinga kama unafanya vizuri. Kuliko kulialia na kulaumu, badilika kwa kuwa haiwezekani hata walio nje ya mpira waone unaboronga lakini wewe unachokiona pekee ni kuwa umegeuzwa dodoki!


2 COMMENTS:

  1. Tatizo lenu mnamsakama Malinzi yeye binafsi, hoja za ukosoaji mwingi Wa vyombo vya habari unamlenga yeye binafsi badala ya kuilenga TFF kama chombo. Hata kama yeye ni kiongozi mkuu lkn ana mipaka nabmaeneo yake kiutendaji. Refa kaboronga lkn lawama analaumiwa Malinzi. Bodi ya ligi imeboronga lawama Malinzi. Kamati ya nidham imeamua vile lawama anashushiwa Malinzi. Kuweni waungwana, uandishi Wa njaa na maslahi ndio unaowapelekea baadhi ya waandishi kumsakama Malinzi.

    ReplyDelete
  2. Tatizo lenu mnamsakama Malinzi yeye binafsi, hoja za ukosoaji mwingi Wa vyombo vya habari unamlenga yeye binafsi badala ya kuilenga TFF kama chombo. Hata kama yeye ni kiongozi mkuu lkn ana mipaka nabmaeneo yake kiutendaji. Refa kaboronga lkn lawama analaumiwa Malinzi. Bodi ya ligi imeboronga lawama Malinzi. Kamati ya nidham imeamua vile lawama anashushiwa Malinzi. Kuweni waungwana, uandishi Wa njaa na maslahi ndio unaowapelekea baadhi ya waandishi kumsakama Malinzi.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic