July 18, 2016


Kocha Msaidizi wa Simba, Mganda, Jackson Mayanja, amesema ana uhakika kikosi hicho kitafanya vizuri msimu ujao kutokana na mbinu zake za ufundishaji kuendana na za kocha mkuu, Mcameroon, Joseph Omog.

Mayanja na Omog wanaendelea na kibarua cha kukinoa kikosi cha timu hiyo ambacho kimejichimbia mkoani Morogoro, kikiendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi baada ya kufanya vibaya msimu uliopita.

Mayanja alisema kutokana na mbinu ambazo wanazitoa kwa kikosi hicho ni wazi kabisa kuwa wana asilimia kubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano watakayoshiriki huku akiwatambia wapinzani wao wajiandae vyema kuwakabili.

“Mwanzoni nilijua tutapata shida katika kufundisha kwa sababu hatukuwa tunajuana lakini baada ya kukaa kwa siku kadhaa, tumeona falsafa zetu zinaendana kwa kuzingatia nidhamu iwe ndiyo kipaumbele kuliko kitu kingine, ambapo pia tumeshaweka mikakati mikubwa ya kuona tunafanikiwa kuifanya Simba iwe timu hatari.


“Naamini tukijumlisha mbinu zangu na Omog, basi timu hii itakuwa tishio sana msimu ujao kama wenyewe tulivyopanga na tunataka kuona makombe yakirejea tena baada ya kuwa na ukame kwa kipindi kirefu sasa,” alisema Mayanja.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV