July 18, 2016


Pamoja na kuwa wa mwisho kwenye msimamo wa Kundi A, Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm ambaye ni kocha bora wa msimu wa 2015-16, amesema wala hawajakata tamaa na badala yake watapambana hadi hatua ya mwisho kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Kauli hiyo, aliitoa kocha huyo mara baada ya kuambulia sare ya bao 1-1 kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Medeama ya Ghana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi katika mtanange ambao walitakiwa kushinda ili wakae pazuri.

Yanga hivi sasa ipo mwishoni katika msimamo huo ikiwa na pointi moja huku TP Mazembe ikiongoza ikiwa na pointi 6 (kabla ya mechi ya jana), MO Bejaia 4 (kabla ya mechi ya jana) na Medeama 2.

 Pluijm alisema kikubwa wanachotakiwa kukifanya ni kutokata tamaa, badala yake kuwapa matumaini wachezaji ili michezo ijayo wapate matokeo mazuri ya ushindi.
Pluijm alisema, anaamini bado wana nafasi nzuri ya kufuzu nusu fainali ya michuano hiyo kama wachezaji wake watapambana na kushinda michezo yote mitatu waliyobakiza.

Aliongeza kuwa, amefurahishwa na viwango vya wachezaji wake wakiwemo viungo kutengeneza nafasi nne za wazi kwa washambuliaji wao walioshindwa kuzitumia.

"Ninaamini kuwa, Yanga bado ina nafasi ya kutinga nusu fainali, ni kama tukishinda mechi zetu zote tatu tulizozibakiza kwenye hatua hii ya makundi.

"Kama tukishinda mechi hizo zote, tutakuwa tumefikisha pointi 10 ambazo zitatupa nafasi kubwa ya kufuzu, hivyo kikubwa kinachotakiwa tukifanye hivi sasa ni kutokata tamaa baada ya sare ya Medeama na badala yake tujiandae na michezo mingine inayofuata.


"Nitakutana na wachezaji wangu kuzungumza nao na kikubwa ni kuwatia moyo na kuwatengeneza kisaikolojia ili tufanikishe malengo yetu,” alisema Pluijm.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic