July 20, 2016

PLUIJM
Bado kukosekana kwa kiungo mkabaji kwenye kikosi cha Yanga, kumezidi kumchanganya kocha Hans van der Pluijm ambaye sasa ameamua kuagiza kupatikana kwa kiungo huyo katika kuimarisha kikosi chake.

Licha ya Yanga kuonekana kukamilika idara nyingi, lakini kiungo mkabaji na beki wa kushoto bado zimekuwa changamoto kubwa kwa Mdachi huyo ambaye amesisitiza kupatikana kwa watu hao haraka.

Inaelezwa tayari kamati ya usajili imeanza kulifanyia kazi suala hilo kwa kuketi kikao mwishoni mwa wikiendi iliyopita kabla na baada ya mchezo dhidi ya Medeama wa Kombe la Shirikisho Afrika uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Beki ya kushoto wa Jangwani inamilikiwa na Oscar Joshua na Mwinyi Haji anayeuguza jeraha lake lakini bado Pluijm ameonekana kutoukubali uwezo wao.

Awali walimuweka kwenye rada Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba, lakini watani wao wakaweka ngumu kumuachia, hivyo wameamua kujipanga upya kuangalia mbadala wake.

Mbali na beki wa kushoto, Pluijm ameagiza kutafutiwa kiungo wa kukaba haraka iwezekanavyo ambaye ataisaidia kwenye michezo inayofuata ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo anaamini bado wana nafasi ya kuchupa nusu fainali licha ya kwamba wapo mkiani mwa Kundi A.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya kamati ya utendaji ya timu hiyo zimeeleza baada ya mechi dhidi ya Medeama, Pluijm alionyesha dhahiri kutoridhishwa na nafasi hiyo.

Hata hivyo jicho la kwanza kwenye kiungo mkabaji limetua kwa nyota wa zamani wa Simba, Abdulhalim Humud ‘Gaucho’ ambaye ni mchezaji huru baada ya mkataba wake na Coastal Union kumalizika.

Licha ya Humud, pia bado hawajafikia muafaka badala yake wanaendelea kuangalia kwingine ikiwa pia ni nje ya nchi.

“Kweli kulikuwa na kikao cha kamati ya usajili kuangalia nani anafaa kulingana na matakwa ya mwalimu. Bado tunajadili baadhi ya mambo kuhusu nafasi hizo (kiungo mkabaji na beki wa kushoto) lakini kimsingi ni lazima zipatikane,” alisema kiongozi mmoja wa Yanga kwa sharti la kutotajwa.

Yanga ilimleta Thaban Kamusoko maalum kucheza kiungo mkabaji lakini ameshindwa kutokana na ‘type’ ya uchezaji wake ya kushambulia ama mchezeshaji huku Said Juma Makapu na Mbuyu Twite wakionekana kushindwa kuhimili nafasi hiyo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV