Klabu ya mpira wa miguu ya Ruvu Shooting ya mkoani Pwani, inayoshiriki ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara(VPL) imetamba kufanya makubwa msimu ujao wa Ligi hiyo na kuwataka mabingwa wa ligi hiyo, Yanga kutarajia upinzani mkali kutoka kwao katika kupigania taji hilo.
Akizungumza kutoka Mlandizi yalipo maskani ya timu hiyo, Ofisa Uhusiano wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, alisema kuwa malengo yao msimu ujao ni kuwa miongoni mwa timu tatu za juu na ikiwezekana kutwaa ubingwa kama walivyofanya Leicester City ya England ambayo msimu uliopita ilipanda daraja na kubeba taji.
Alisema kuwa kikosi chao kipo katika maandalizi kabambe na kwamba Jumatatu wanatarajia kutambulisha wachezaji wao, wakati watakapovaana na Mbeya City katika mchezo wa kirafiki utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi.
“Baada ya kupanda daraja, matarajio yetu ni kucheza kandanda maridadi kama ilivyo kawaida yetu, lakini pia kupambana ili tuweze kuwa katika nafasi za juu, hivyo hizo timu zinazojiita kubwa, yaani Simba na Yanga, zikae chonjo,” alisema Bwire.
Alisema kwamba kwa jinsi wanavyojipanga, iwapo waamuzi watazingatia sheria zote 17 za soka, ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu ujao lazima utue Mlandizi yalipo maskani yao.
Akiuzungumzia udhamini wa ligi hiyo, alisema angalau unawasaidia kufanikisha ushiriki wao wa ligi hiyo kwenda vizuri, japo wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali.
Aliipongeza kampuni ya Vodacom Tanzania ambao ni wadhamini wa ligi hiyo kwa kuendelea kudhamini ligi hiyo na kuboresha sehemu ya udhamini wao kila mara,Pia aliitaka kampuni hiyo kuangalia kama wanaweza si tu kuwahisha kuwapa fungu la maandalizi ya ligi, lakini pia kuongeza kiwango zaidi kwa mkataba ujao ili timu nyingi zinazoshiriki ligi hiyo zisiwe zinapata usumbufu wa kujiendesha.
0 COMMENTS:
Post a Comment