July 15, 2016


Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm, ameshusha presha ya mechi dhidi ya Medeama ya Ghana mara baada ya kuhakikishiwa kuwa mshambuliaji wake Mrundi, Amissi Tambwe amepona na ni ruksa kumtumia kwenye mchezo huo.

Yanga iliyoweka kambi yake Bahari Beach Hotel, Dar, inatarajiwa kuvaana na Medeama, kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Pluijm alisema mshambuliaji huyo ana umuhimu mkubwa wa kucheza katika mechi hiyo kutokana na mfumo anaotarajiwa kuutumia ndani.

Amesema hofu ya kumkosa Tambwe imeisha baada ya mchezaji huyo kuanza mazoezi mepesi ya binafsi juzi asubuhi kwenye Uwanja wa Boko Beach Veteran, Dar.

Aliongeza kuwa anaheshimu uwezo wa wachezaji wake wote, lakini anamhitaji Tambwe kuwepo kwenye kikosi hicho kutokana na kuzoeana na Ngoma wakiwa uwanjani.

“Daktari wa timu amenihakikishia kuwa ataweza kucheza mechi hiyo ya Medeama kutokana na maendeleo ya kiafya kuwa vizuri.

“Ninaamini uwepo wake kwenye timu utachangia ushindi wa mchezo kutokana na umuhimu wake kwenye timu,” alisema Pluijm.

Upande wa Tambwe alipoulizwa juu ya afya yake na mchezo huo wa kesho, alisema: “Nashukuru ninaendelea vizuri, hatma yangu ya kucheza namuachia kocha, lakini mimi nimepona na ningetaka kucheza katika mechi hiyo ambayo lazima tuwafunge kwa staili yoyote ili kuhakikisha tunatimiza ahadi yetu ya kufika nusu fainali ya michuano hiyo.” 


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic