July 15, 2016


Na Saleh Ally
MASHABIKI wa soka nchini walikuwa wakiuliza kila mara kuhusiana na kama uongozi wa Yanga kwa mara nyingine utaamua kutangaza hakutakuwa na kiingilio wakati timu yao itakaposhuka dimba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kuwavaa Medeama ya Ghana.

Kuhoji huko kulitokana na uamuzi wa uongozi wa Yanga kuamua kutangaza kiingilio hakitakuwepo wakati timu hiyo ilipoivaa TP Mazembe. Mashabiki walijitokeza kwa wingi hadi kukawa hakuna nafasi.

Safari hii, Yanga wametangaza kiingilio na wako mashabiki waliolalamika! Kwa kuwa wangependa kuona bure kwa mara nyingine. Mimi naona pia, ile bure moja inatosha na huenda isije tena au ikitokea basi iwe baada ya kipindi kingine kirefu.
Takribani, miaka kumi iliyopita, Yanga kupitia Yusuf Manji ambaye wakati huo alikuwa mfadhili ilitangaza kutokuwa na kiingilio wakati timu yake ilipokuwa ikiivaa El Merreikh ya Sudan kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Imerudia tena mwaka huu. Hivyo, kuingia bure haliwezi kuwa suala muhimu sana la kujadiliwa.

Tunajua liliwakwaza sana TFF ambao wameonyesha mambo mengi yasiyokuwa na msingi katika kipindi hiki na hayakupaswa kufanywa na mtu anayeweza kupewa jina la mzazi au msimamizi mkuu wa kitu fulani. Ninaamini kuna ambayo waliyafanya kwa jazba na mwisho yameisha hovyo kabisa kwa kuonyesha wao ni watu waliofanya mambo yao bila kupima na si sahihi.

Tuachane na TFF maana hawajawahi kuwa sehemu ya kuongeza nguvu ya ushangiliaji iwe Yanga, Simba, Azam FC au timu yoyote inacheza kuliwakilisha taifa letu, badala yake wao wanafaidika kwa kuwa wana asilimia za mapato.

Nijadili na mashabiki ambao watakwenda Uwanja wa Taifa wakati Yanga inaivaa Medeama ya Ghana katika mechi yake muhimu kabisa ya Kombe la Shirikisho. Yanga inatakiwa kushinda mechi hiyo, ikifungwa rasmi itakuwa ni mwakilishi tu katika michuano hiyo.

Mashabiki walioingia bure kwenye mechi dhidi ya TP Mazembe, licha ya wingi wao hawakuwa na msaada mkubwa wa Yanga na wakafunikwa hata na mashabiki wachache kabisa wa TP Mazembe hata kama walipata msaada kwa wale wa Simba ambao walipenda Yanga ifungwe.

Kama ungechanganya wale mashabiki wa Simba na wale wa Mazembe, bado hawakuwa na nafasi hata kidogo kuwafunika wale wa Yanga ambao walikuwa wengi zaidi ya mara tatu yao. Ajabu, walionekana wanaoshangaa na wasiojua la kufanya.

Yanga walikuwa na nafasi kubwa ya kufanya vizuri, hivyo walikuwa na mengi ya kufanya washangiliwe siku hiyo. Lakini haikuwa hivyo kwa kuwa mashabiki hapa nyumbani Tanzania wanajua kushangilia pale kunapokuwa na tukio tu, mfano mchezaji kakosa bao, kipa kaokoa au vinginevyo.

Wengi hukaa kimya na muda mwingi kuutumia kulalamika, kufundisha au kuonyesha kundi walilokaa nalo karibu kwamba wao wanajua sana. Pale jukwaani, si mahala pake, pale ni kushangilia na kuisaidia timu kama mchezaji wa 12.

Yanga imewakumbuka tena mashabiki, imeweka hadi kiingilio cha Sh 3,000 ambacho ni cha chini zaidi na lazima tukubali kwamba wamejitahidi katika hilo.

Kikubwa ni Wanayanga na wapenda michezo na mpira, wajitokeze kwa wingi. Huu ni wakati wa kuonyesha kwamba mashabiki wanaweza kuwa msaada na kudhihirisha ile zana ya kucheza nyumbani inafaida kwa kuwa mwenyeji anakuwa anapata msaada kutoka kwa mashabiki wake wanaokuwa wengi.

Kama Yanga haiwezi kushangiliwa kwa nguvu nyumbani. Tofauti yake na kucheza ugenini, inapotea. Hivyo lazima mashabiki watakaofanikiwa kufika uwanjani, wabadili upepo kutoka ule wa bure ambao walichemsha kushangilia na huu wanaolipa kidogo na washangilie kuwachanganya Waghana, inawezekana kabisa.

Kwenda uwanjani kama shabiki, halafu ukakaa jukwaani ukiwa kimya, ni kumuonyesha mchezaji aliye uwanjani kuna mashabiki wengi waliojitokeza lakini si wale wanaotuunga mkono. Unaweza kuifananisha na kauli hii; “kujishambulia mwenyewe.”
0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV