July 6, 2016

KERR

Aliyekuwa Kocha wa Simba, Muingereza, Dylan Kerr, amemtumia salamu za pongezi kocha mpya wa timu hiyo, Mcameroon, Joseph Omog, baada ya kufanikiwa kupewa mkataba wa miaka miwili ya kukinoa kikosi hicho kwa msimu ujao.

Tangu Kerr atimuliwe kazi ndani ya Simba Januari, mwaka huu, klabu hiyo ilikuwa ikimsaka mbadala wake huku ikimpa jukumu la kukisimamia kikosi hicho, Mganda, Jackson Mayanja ambaye alikuwa peke yake kama kocha msaidizi.

Omog, hii si mara yake ya kwanza kufundisha soka Tanzania, kwani msimu wa 2013/14, alikuwa akiinoa Azam FC na kufanikiwa kuiongoza mpaka ikachukua taji la Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza mchezo.

Kerr ambaye tangu aondoke Tanzania mpaka sasa hajapata timu ya kuinoa, amesema kuwa: “Kiukweli simjui huyo kocha lakini ningependa kumpongeza kwa hatua hiyo aliyofikia kwani makocha wengi walikuwa wanaitaka nafasi hiyo ambayo yeye ameipata.


“Kikubwa watu wanataka kuona atafanya nini kwa msimu ujao kwani Simba inataka mafanikio waliyoyakosa kwa muda mrefu, tusubiri tuone kitakachojiri.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV