July 6, 2016


Beki na aliyekuwa nahodha wa kikosi cha Simba, Hassan Isihaka amefunguka kuwa mpaka sasa hajui hatma yake ndani ya timu hiyo kutokana na kutofuatwa na kiongozi yeyote kwa mazungumzo huku tetesi zikidai viongozi wake wapo kwenye harakati za kumpeleka kwa mkopo Mbao FC.

Isihaka ambaye hakuwa na maelewano mazuri na na aliyekuwa kocha, Mganda, Jackson Mayanja katika msimu uliopita  amekuwa akihusishwa kutolewa kwa mkopo ndani ya timu hiyo kutokana na mabosi wa timu hiyo kutoridhishwa na kiwango chake.

Isihaka alifunguka kuwa mpaka sasa bado hajafanya mazungumzo na kiongozi yeyote yule kwa ajili ya kuangalia hatma yake ndani ya klabu hiyo na kama wanataka kumtoa kwa mkopo ni heri wamwambie atafute timu ya kuichezea mapema.

“Wao bado hawajanifuata na mimi niko njia panda kwani sifahamu lolote juu ya maisha yangu ya Simba kama nitakuwepo kwenye timu katika msimu ujao ama la, lakini ni bora waniambie mapema nijue nachukua maamuzi gani.


“Nasikia tu tetesi kuwa wanataka kunipelekea Mbao FC ya Mwanza, lakini kwangu sidhani kama nitaenda huko kwa sababu mchezaji ndiye anayechagua wapi aende sasa kama wao wamepanga kunipeleka huko wataenda kucheza wenyewe,” alisema Isihaka.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV