July 30, 2016


HII sasa ni kufuru kwani mfanyabiashara mkubwa nchini, Mohamed Dewji ‘MO’ amesema yupo tayari kutoa Sh bilioni 20 kuwekeza katika Klabu ya Simba ili ipate mafanikio.

MO amesema anaweza kufanya hivyo endapo tu timu hiyo itakubali kubadili mfumo wake na kujiendesha kama kampuni.

Kwa mujibu MO, mfumo huo ndiyo utakaomuwezesha kununua hisa asilimia 51 kwa Sh bilioni 20 ambazo zitatumika kwa mambo mbalimbali ya kimaendeleo yatakayoifanya Simba kupata mafanikio.

MO ambaye ni Mbunge wa zamani wa Jimbo la Singida Mjini na Rais wa Makampuni ya Mohamed Enterprises Limited (MeTL), hivi karibuni alitangaza kununua hisa za Simba lakini suala hilo linaonekana kuwa gumu kutokana na mfumo wa sasa wa klabu hiyo.

MO amesema kutokana na mapenzi yake kwa Simba, ameamua kutoa Sh bilioni 20 endapo uongozi wa Simba chini ya Rais Evans Aveva utakubali kumuuzia asilimia 51 ya hisa za umiliki wa klabu hiyo.

“Zipo Sh bilioni 20 nilizotenga kuipa Simba endapo uongozi utakubaliana na wanachama kubadili mfumo na timu kuwa kampuni, kiasi hicho nitakitumia kununua hisa,” alisema MO.

MO amefafanua kwa kusema, ndani ya fedha hizo yafuatayo yatafanyika Simba;

BAJETI ZAIDI YA MANJI
MO alisema ndani ya Sh bilioni 20 atakazotoa, Simba itapata Sh bilioni 5 kwa mwaka, bajeti ambayo itakuwa mara mbili kwa ile ya Yanga ambayo ni Sh bilioni 2.5. Yanga ipo chini ya Mwenyekiti Yusuf Manji ambaye amekuwa akitoa mfukoni kiasi hicho cha fedha.

“Lengo langu ni kuitoa Simba kwenye bajeti ya Sh bilioni 1.2 hadi kufikia Sh bilioni 5 ambazo nitazitoa kila mwaka na kuzizidi Yanga na Azam ambazo zinatumia Sh bilioni 2.5,” alisema MO.

UWANJA, HOSTELI, USAJILI WA MAANA
Chini ya uwekezaji wake, MO alisema atahakikisha Simba inakuwa na uwanja wa kisasa, hosteli zenye kila kitu muhimu kwa mchezaji kama gym, mabwawa ya kuogelea na viwanja vizuri vya mazoezi pia atafanya usajili wa maana.

“Simba ilianzishwa mwaka 1936 lakini haina uwanja wa maana wa mazoezi hata mechi zaidi ya kukodi, tazama Azam imeanzishwa juzi tu lakini wana kila kitu.

“Soka la sasa ni la kisasa, nitahakikisha Simba inakuwa na uwanja wake, hosteli za maana zenye kila kitu muhimu kwa mchezaji halafu tutaweza kufanya usajili wenye tija kwa timu ambao utakuwa ni wa gharama kubwa,” alisema MO.

WANACHAMA KUMILIKISHWA TIMU
MO amesema timu ikibadili mfumo kwa wanachama kukubali kumuuzia hisa asilimia 51 za umiliki, atapendekeza hisa zinazobaki wapewe wanachama wenye muda mrefu ndani ya timu.

“Kwa kuwa timu itakuwa kampuni tayari, wanachama watapewa hisa na kutakuwepo na gawio lao kila mwaka kutokana na faida itakayopatikana, sasa uamuzi utakuwa wa mwanachama kama anabaki na hisa au anauza.

“Hizo Sh bilioni 20 zitakaa benki kwenye akaunti maalumu kwa muda wa miaka mitano tutapata faida ya asilimia 17.5 ambayo ni sawa Sh bilioni 3.5,” alisema MO.

ATOA MAMILIONI KUSAJILI KIFAA CHA IVORY COAST
MO bila kumtaja jina, alisema alipata taarifa za Simba kutaka kumsajili mchezaji kutoka Ivory Coast lakini inashindwa kufanya hivyo kutokana na tatizo la fedha, yeye ameahidi kulitekeleza hilo.

“Mambo yakienda sawa na mfumo ukibadilika hakuna shida nitatoa fedha za kumsajili mchezaji huyo bila tatizo, mimi nataka kuona Simba inarudi katika makali yake siyo kama ilivyo sasa.

“Naamini tukisajili vizuri mambo yatakuwa mazuri ndani ya uwanja na Simba itakuwa kali isiyochezewa na kila mtu, naamini wanachama na viongozi watakubaliana nami na kufanya mabadiliko,” alisema MO.

MKUTANO MKUU SIMBA KESHO
Wakati MO akitangaza kutoa kiasi cha Sh bilioni 20 kwa Simba kama ikikubali kufanya mabadiliko ya kuwa kampuni, klabu hiyo kesho Jumapili itafanya mkutano mkuu wake kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi, Masaki jijini Dar es Salaam.

Moja kati ya mambo yanayosubiriwa kujadiliwa katika mkutano huo ni ishu hiyo ya MO kutaka kununua hisa ambapo wanachama wataelekezwa maana ya hisa pia kuulizwa kama wanaridhia mchakato huo au la.

Hata hivyo, Rais wa Simba, Evance Aveva ametilia mkazo kuwa ni wanachama hai tu ambao wataruhusiwa kuhudhuria mkutano huo muhimu kwa maendeleo ya klabu.

“Kutakuwa na ajenda nyingi, naomba wanachama hai wajitokeze kwa wingi na wale ambao hawajalipia kadi watalipia palepale ukumbini lengo tukutane wote na kufanya mkutano,” alisema Aveva.

Licha ya MO kusema amewahi kukutana na viongozi wa Simba zaidi ya mara moja ili kuwekeza Simba, Aveva yeye amesema hawajawai kukutana na mfanyabiashara huyo.
Hata hivyo, wanachama wa Simba kesho watakuwa na nafasi ya pekee kujadili mchakato huo wa MO kutaka kununua hisa za klabu hiyo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV